Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Kamishna wa Polisi Diwani Athumani ameongea na Vyombo vya habari akiwataka wananchi kuongeza kasi kusoma alama za nyakati maana serikali ya awamu hii sio salama kwa wala Rushwa.
Akiwa Mkoani Kagera jana October 1, CP Diwani alisema kuwa TAKUKURU inayoongozwa na yeye itatekeleza wajibu wake kwa kuzingatia Sheria haitaangalia itikadi, hadhi au cheo ulichonacho, atakayejihusisha na vitendo vya Rushwa hatabaki salama.
Diwani alisema atahakikisha anawaburuza mahakamani watuhumiwa wote wa vitendo vya rushwa mapema sheria ichukue mkondo wake.
Pia aliwahadharisha watumishi wa umma kuwa makini na uadilifu wao katika maeneo ya kazi kwa vile sasa nyakati zimebadilika Serikalini.
Alisema kutokana na Rais Magufuli kueleza kutoridhishwa na namna washukiwa wa vitendo vya rushwa wanavyoshughulikiwa, jukumu lake kubwa la haraka ni kuwafikisha mahakamani watu wote waliotajwa au kuripotiwa Takukuru.
Alisema watumishi wanapaswa kubadilika na kufanya kazi kwa weledi na kutumia muda wa kazi vizuri kwani Serikali hii haina mzaha.
“Huu si wakati wa mtumishi wa umma kujilimbikizia mali kiujanja ujanja. Kila mtumishi wa umma aridhike na anachokipata na afanye kazi kwa bidii ili kuunga mkono jitihada za Rais Magufuli katika kuhakikisha fedha za umma zinatumika kwa shughuli za maendeleo.
“Katika uongozi wangu nitahakikisha natumia juhudi zangu zote kwa ushirikiano na viongozi wenzangu wanaopiga vita rushwa kuhakikisha Tanzania bila rushwa inawezekana,” alisema.
Alisema rushwa ni adui mkubwa wa haki ambaye hapaswi kufumbiwa macho kwani imekuwa inarudisha nyuma maendeleo ya wananchi na kuwaathiri wananchi wanyonge.
“Niko tayari kupambana na nina imani hii vita nitaishinda. Wanaojipanga kuchukua rushwa au kutoa rushwa wajipange upya,” Diwani alionya.
Alisema Takukuru imejiwekea malengo kuona miradi yote inatekelezwa haraka na kwa ufanisi na kukamilisha utafiti wao kuhusu mazingira ya rushwa na kuomba ushirikiano wa wananchi.
“Takukuru peke yetu hatuwezi kufanya kazi peke yetu. Tunahitaji ushirikiano wa wananchi wote. Mfano nimeona kuna mianya mikubwa ya rushwa kwa wafanyabiashara wanaotumia mashine za EFDs.
Kiwango wanachoandika kwenye risiti hakiendani na bidhaa wanazouza.
“Hawa inabidi tule naosahani moja. Nakemea wale wote wanaochukua asilimia fulani kabla ya mkandarasi hata hajatekeleza mradi,” alisema.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Brigedia Jenerali Marco G aguti alimpongeza Diwani kwa kuteuliwa akisema hana shaka na uwezo wake kusimamia masuala makubwa ya kitaifa.