Chadema Yafunguka Sababu Zinazosababisha Wizi wa Mitiani kwa Walimu

Chadema Yafunguka Sababu Zinazosababisha Wizi wa Mitiani kwa Walimu
Waziri Kivuli wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi Suzan Lyimo amesema kuwa  mazingira magumu ya walimu ikiwemo malimbikizo ya mishahara na changamoto zinazowakabili katika utekekelezaji wa majukumu yao ndio chanzo cha kufanya vitu kinyume na maadili ikiwemo wizi wa mitihani.


Akizungumza na wanahabari katika maadhimisho ya siku ya walimu duniani, Lyimo amesema kuwa hakuna nchi inayoendelea duniani bila kuwekeza kwa walimu, na kusisitiza kuwa Tanzania ya viwanda haiwezi ikawezekana kama serikali haitawekeza kwenye sekta ya elimu.

Lyimo amesema kuwa walimu ndiyo kila kitu katika kumjenga mwanafunzi au kumporomosha, mwalimu akiwa na matatizo ya muda mrefu hasa kimaslahi hawezi kuandamana barabarani bali ataandamana moyoni na matokeo yake ni kama kilichotokea wilayani Chemba.

"Inaudhi na linasikitisha, niseme tu jambo hili linatoa taswira ya kuwa walimu wamechoshwa na changamoto zilizopo hasa za kupandishwa madaraja, mwalimu akipandishwa daraja na akiwa analipwa vizuri sidhani kama wizi wa mitihani ungetokea, nimekuwa nikipiga kelele bungeni lakini bado elimu haijapewa kipaumbele", amesema Lyimo.

Katika maadhimisho haya leo Oktoba 5, Chama cha Waalimu Mkoa wa Dar es salaam kimeitaka serikali kuwalipa waalimu 13,127 madai yao zaidi ya shilingi Bilioni nne na milioni mia sita ambazo walistahili kulipwa baada ya kuhakikiwa madai yao ya Januari 2018.

Malalamiko hayo yametolewa na Abdallah Mkaula ambaye ni katibu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT)  Mkoa wa Dar es salaam, ambapo pia wanaitaka serikali kushugulikia Upungufu wa vyumba vya waalimu, vyoo, upungufu wa vitabu vya kifundishia, kiada na ziada, uwingi wa wanafunzi ambapo darasa moja laweza kuwa na wanafunzi 100 hadi 200, pamoja na upungufu wa madawati

Hayo yanajiri ikiwa ni siku chache tangu Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) limetangaza kuyafuta matokeo ya mitihani ya Darasa la saba kwa shule za msingi zote zilizopo ndani ya Halmashauri ya Chemba, pamoja na baadhi ya shule katika halmashauri ya Kondoa, Kinondoni, Mwanza jiji na Ubungo kwa kosa la kuhusika kwa kuvujishakwa mitihani ya darasa la saba ikiwa ni kinyume na taratibu na kanuni za mitihani nchini.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad