Baraza la Wazee wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) limesema hatua ya baadhi ya viongozi na wanachama wa vyama vya siasa kuhamia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kunatokana na shinikizo kutoka katika chama hicho tawala.
Wakizungumza na waandishi wa habari wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wazee Kimataifa, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Chadema, Hashim Juma Issa, na katibu wake Roderick Lutembeka wamesema baadhi ya viongozi huzushiwa kesi kwa lengo la kuwatishia ili wahamie chama tawala.
Katibu wa baraza hilo Roderick Lutembeka amesema Chadema inaposema wabunge na madiwani wao wanaoamia CCM wananunuliwa inao ushahidi.
"Suala la ushahidi wa wabunge na madiwani kununuliwa tunao na tuliwahi kutoa ushahidi wa mkuu mmoja wa wilaya akizungumza na kupanga mipango yote. Ushahidi huo tuliupeleka Takukuru lakini ukafunikwa funikwa," amesema Lutembeka na kuongeza;
"Kuna mtu kahamia juzi tu hapa, kafika huko kaanza kufanya mambo ya ajabu, kuna kijana mmoja alichukua mkopo alikuwa rafiki wa huyo mtu, alikuwa akimlazimisha ahamie huko ushahidi wa ushawishi huo tunao"