Ushindi wa jumla ya goli 3-2 ikiwa ni mchezo wa mwisho kabla ya kuelekea katika mapumziko kupisha michuano mbalimbali katika timu za taifa ikiwemo michezo ya kirafiki umekuwa mchungu kwa kocha wa Manchester United Mreno Jose Mourinho.
Ushindi umekuwa mchungu kwa sababu ameshtakiwa na chama cha soka nchini Uingereza kutokana na kauli yake aliyoitoa baada ya mchezo huo ambao alikutana na Newcastle United katika dimba la Old Trafford.
Jose Mourinho ameshtakiwa na Chama hicho cha Soka juu ya kile alichokiongea baada ya ushindi huo wa Ligi Kuu wa timu yake ya Manchester United dhidi ya Newcastle mnamo Oktoba 6, Inadaiwa Meneja huyo wa United alizungumza kwenye kamera baada ya timu yake kutoka nyuma na kushinda katika mchezo huo.
Taarifa ya FA inasomeka hivi: “Inasemekana kwamba lugha yake mwishoni baada ya matokeo hayo, kama ilivyotumwa na kuonekana katika video na picha mbalimbali, ilikuwa ya dharau, matusi na ikionekana isiyofaa kabisa, Hivyo Mourinho anatakiwa kujibu tuhuma hizi hadi ifikapo Octoba 19 muda wa saa kumi na mbili jioni”
Lakini pia Mreno huyo anaweza kukumbwa na tuhuma nyingine endapo atapatikana na hatia ya kugusa mstari wa uwanja wakati mchezo huo ukiendelea.
Yote haya yanakuja kutokana na hali ya Mournho na uongozi wa United ya kutokuelewana na ilikuwa ikisemekana Mreno huyo angefukuzwa endapo angepoteza mchezo huo,kwahiyo baada ya goli la ushindi lililofungwa na Sanchez lilionekana kama ni mwokozi kwa meneja huyo na baada ya mchezo kumalizika alionekana akiongea neno mbele ya kamera wakati anaelekea katika vyumba vya kubadilishia nguo wakati wa filimbi ya mwisho ya mchezo.
Wikendi hii ya tarehe 20 Octoba United itasafiri hadi katika jiji la London kukabiliana na Chelsea moja ya timu iliyoanza vizuri msimu huu ikiwa katika nafasi ya pili ikijikusanyia alama 20 nyuma ya bingwa mtetezi Manchester City wenye alama 20 pia ila zikitofautiana kwa wingi wa magoli ya kufunga na kufungwa huku United ikiwa katika nafasi ya 8 ikiwa na alama 13.