Jeshi la Polisi mkoani Mbeya limethibitisha kuwakamata, kuwahoji na kuwaachia kwa dhamana mbunge wa Busega (CCM), Dk Raphael Chegeni na Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha kwa madai ya kuharibu mali za mwekezaji raia wa Ujerumani.
Kamanda wa Polisi wa mkoani humo, Ulrich Matei amesema wawili hao walikamatwa jana, kuhojiwa na kuachiwa kwa dhamana.
Amesema polisi walipata taarifa kutoka katika ubalozi wa Ujerumani kwamba kuna mabaunsa 20 wamevamia nyumba ya mwekezaji huyo mwenye mashamba ya parachichi.
“Masha na Chegeni walikuwa wanatimiza wajibu wao kwa mujibu wa Mahakama ya kumuondoa mwekezaji huyo katika eneo lile,” amesema Matei.
“Hata hivyo hawakufuata utaratibu ikiwemo kumpa taarifa mhusika na haikuwa siku ya kazi. Kama yule Chegeni ni mbunge angetumia utaratibu hata kupitia kwa mkuu wa mkoa kuliko kufanya kama vile.
Amebainisha kuwa walipopata taarifa kutoka ubalozi wa Ujerumani ziliwashtua kwa sababu Tanzania ni nchi ya amani.
Kwa mujibu wa Kamanda Matei, polisi walipofika eneo hilo walikuta baadhi ya vitu vimeharibiwa huku mwekezaji huyo ambaye ni mwanamke akijeruhiwa sehemu mbalimbali mwilini.