Christopher Mwakasege "Pamoja Na Msiba Huu Mzito Kwetu, Bado Utabaki Kuwa Mungu na Tutaendelea Kukutumikia"


Mwalimu Christopher Mwakasege ameongoza maombi kwa zaidi ya dakika 30 wakati wa ibada ya kuaga mwili wa mwanaye wa pekee wa kiume, Joshua aliyefariki dunia Oktoba 11, 2018 baada ya kuugua ghafla akiwa kazini.


Ibada hiyo ya mazishi imefanyika leo Jumanne Oktoba 16, 2018 katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) Mbezi Beach na kuhudhuriwa na mamia ya watu, akiwemo Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.


Akiwa amesimama mbele ya jeneza lenye mwili wa mwanaye, Mwakasege aliongoza maombi hayo baada ya waombolezaji kumtaka kuzungumza.


Huku akiwaomba wanaotaka kuokoka kupita mbele ya kanisa Mwakasege amesema, “Hata kama najiuliza maswali magumu bado utabaki kuwa Mungu wangu, sitaacha kuimba ni salama moyoni mwangu.”


Akizungumzia mazingira ya kifo cha mwanaye, Mwakasege amesema haikuwa rahisi kupokea taarifa hizo ila alilazimika kuendelea na semina ya siku tatu iliyokuwa inafanyika jijini  Mbeya.


Amesema kabla ya mwanaye kukutwa na mauti waliwasiliana na alimuahidi kuwa wangezungumza tena jioni baada ya kumaliza semina.


“Baada ya kumaliza semina nilimpigia simu lakini iliita bila kupokelewa. Baadaye mlinzi wa kazini kwao alipokea na akatueleza kuwa  Joshua amekimbizwa hospitali," amesema Mwakasege.


“Baadaye nilipigiwa simu na daktari na alinieleza kuwa mwanangu amefariki dunia. Ilikuwa ngumu kupokea taarifa ya daktari aliyenieleza kuwa walijitahidi kumuhudumia lakini ilishindikana.”


Amesema, “Kitu cha kwanza niliwaza namna ya kumshirikisha mke wangu kwa sababu wakati huo alikuwa akimuombea Joshua.”


Amesema hatua ya kwanza ya kumueleza mke wake ilifanikiwa na kubakiza jambo moja la iwapo aendelee na semina ama la.


“Kwa sababu taarifa za kifo zilikuja usiku tulikaa hoteli  tuliyokuwa tumefikia hadi usiku tulijiuliza tutamueleza  nini Mungu katika hali ile.  Tuliwaza watu zaidi ya 10,000 waliokuja kuhudhuria semina na tukaona tufikilie zaidi semina," amesema Mwakasege.


Huku akizungumza kwa umakini Mwakasege amesema, “haijalishi sehemu tunapita tunataka kukuhakikishia Mungu pamoja na jambo hili gumu utabaki kuwa Mungu kwetu. Tutaendelea kukutumikia na hatutakukasirikia.”


Amesema waliwashirikisha ndugu na kuwaeleza kuwa licha ya kifo cha Joshua, wataendelea na semina kwa siku tatu zilizobaki.


Amesema japo watu walikuwa na taarifa za kifo cha Joshua ila hawakusema chochote na waliendelea na semina hadi juzi Jumapili.


“Siku ya mwisho (ya semina) ndio nilitangaza kuhusu kifo cha Joshua nilikuwa namuita bwana mdogo. Nina ujumbe mwingi  sikuweza kusoma. Niwaombe tu radhi wote walionitumia ujumbe nikitulia nitasoma,” amesema Mwakasege.


Amesema aliwaeleza binti zake watatu kuhusu kifo cha Joshua na walimuuliza kuhusu semina kama ataendelea nayo au atasitisha.


Amesema pamoja na familia yake wanamshukuru Mungu kwa kuwa tangu wakianza huduma hiyo waliahidi kuwa watamtumikia Mungu siku zote za uhai wao.


Maziko ya Joshua yatafanyika Jumatano Oktoba 18, 2018 Tukuyu jijini Mbeya.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad