Kampuni ya IPP imetangaza kuanza ujenzi wa kiwanda cha kwanza cha kutengeneza simu janja maarufu kama smartphone, simu zitakazokuwa na uwezo wa kukaa na chaji kwa muda wa wiki moja na kwa wasiokuwa na umeme wanaweza chaji kwa nguvu ya Jua.
Kiwanda hicho kitakachokuwa cha kwanza nchini na Afrika Mashariki, kitajengwa eneo la Mikocheni jijini Dar es salaam, ambapo uwekezaji wake ukikadiriwa kuwa ni shilingi bilioni 11 na kitaanza uzalishaji ndani ya miezi mitatu ijayo, kikitarajia kuajiri takribani watu elfu mbili.
Akizungumza na wanahabari Mwenyekiti Mtendaji wa makampuni ya IPP Dkt. Reginald Mengi amesema kiwanda hicho kitakuwa na mchango mkubwa kwenye uchumi na sehemu kubwa ya watakaoajiriwa ni watu wenye ulemavu.
"Simu zitakazotengenezwa na IPP TouchMate zitakuwa na uwezo wa kukaa na chaji kwa muda wa wiki moja na lengo litakuwa ni kuendana na mazingira ya maisha halisi ya Tanzania", amesema Dkt. Mengi.
Tayari ufungaji mitambo kwenye kiwanda hicho kitakachojulikana kama IPP TouchMate umeshaanza ambapo mbali ya simu, bidhaa nyingine zitakazotengenezwa ni pamoja na Tablet, Kompyuta mpakato, headphones pamoja na bidhaa za kielektroniki za majumbani pamoja na vipuri vyake.