Eric Shigongo Aeleza A-Z Chanzo cha Bifu Lake na WCB, Amtaja Wema na Diamond



Mjasiriamali na mwaandishi wa vitabu, Eric Shigongo ambaye alikuwa mmoja kati ya wageni waalikwa kwenye tukio la Diamond kutoa misaada Tandale, amefunguka kuzungumzia chanzo cha ugomvi wake na uongozi wa WCB.



Shigongo ametoa kauli hii:

Shigongo amedai kauli yake ya kwamba uongozi wa WCB ulikuwa unampeleka shimoni Diamond Platunumz kutokana na kuzipiga chini  show nyingi za ndani na kufanya za nje tu, ilikuwa ina lengo la kumfanya muimbaji huyo aone kuna umuhimu wa kuwathamini watanzania ambao wamemfanya afike hapo alipofikia.

Takriban miaka mitatu iliyopita mimi na wafanyakazi wenzangu katika Kampuni ya Global Publishers tunayofanyia kazi tulikaa chini na kuamua kufanya tamasha la kurejesha kwa jamii iliyotufikisha hapa tulipo, tukachagua eneo la watu wa kawaida liitwalo Tandale jijini Dar es Salaam, ambako ilitokea kukawa ndiko ambako msanii maarufu Diamond Platnumz anatokea.

Tamasha lililoitwa Twen’zetu Ubilioneani liliandaliwa kwenye Uwanja wa Maguniani-Tandale vilivyoko katikati ya eneo la Tandale, kwa sababu Diamond anatokea huko, tuliamua kumwomba aungane nasi pamoja na wasanii wengine kama Roma Mkatoliki, Baby Madaha na kundi lake na wengine wengi ambao walitumbuiza na kuwafundisha watu wa Tandale mbinu za kutoka kwenye umaskini.

Diamond ambaye jina lake halisi ni Nasibu Abdul, hakukataa, aliungana nasi na tukafanya kazi hiyo kwa uaminifu kabisa, Watanzania wengi wataikumbuka shoo hiyo kwa sababu ilizaa matunda mengi na zipo shuhuda za watu ambao leo hii wanamiliki biashara zao kwa sababu tu walihudhuria tamasha lile na kutiwa moyo.

Lengo lilikuwa ni kumfanya mtu aliyezaliwa katika familia na mazingira ya umaskini aamini kwamba kuzaliwa maskini siyo kufa maskini, kila mwanadamu anao uwezo wa kufika mahali popote maishani mwake kiuchumi, kielimu na kadhalika kama tu ataamua na kufanya uamuzi sahihi, tulitoa shuhuda zetu pale, kuonesha tulikotokea, mambo tuliyoyafanya ili kuwafanya vijana waamini inawezekana kabisa kupanda hadi juu kimaisha.

Lazima nikiri kwamba halikuwa wazo la kwanza duniani, mimi pia niliiga kwa wasanii wa Kimarekani kama Snoopy Dog Doggy, mwigizaji wa sinema na mwanamuziki Tyrese Gibson wanaoishi katika maeneo ya watu matajiri katika Jiji la Los Angeles, kama vile Beverly Hills na Hollywood, lakini mara kadhaa hurejea maeneo ya watu maskini ya South Central ambako wanaishi watu weusi maskini kutoa misaada na kuwahamasisha ili wajikwamue kama walivyojikwamua wao.

Kukumbuka ulikotoka ni jambo jema sana na hufungua sana baraka kutoka kwa Mungu kwani katika vitabu vyake vitakatifu yeye husema; “Nitakubariki ili ufanyike baraka kwa watu wengine.” Sababu ya kumchukua Diamond Platnumz, msanii ambaye ninaamini amefanikiwa sana kimuziki akitokea kwenye umaskini kama maisha ya watu wengi yalivyo kwenda naye Tandale, ilikuwa njia ya kumkumbusha juu ya umuhimu wa kugawana na watu alichopewa na Mungu.

Namfahamu Diamond kama kijana mtiifu, mkarimu mwenye heshima na adabu, asiyependa ugomvi na watu wanaomzidi umri, Mungu shahidi yangu, watu wawili tu katika nchi hii ambao magazeti yanaweza kuwaandika, lakini wasipige simu kutukana wahariri au waandishi, nao ni Diamond Platnumz na Wema Sepetu.

ilichokuwa kikinishangaza kama tabia ya Diamond ilikuwa hiyo, kwa nini sasa alikuwa harejei sana alikotoka kuwakumbuka aliowaacha nyuma? Jambo moja lililokuwa likinisumbua zaidi moyoni mwangu ni kwamba Diamond alikua na mashabiki wengi mno Tanzania, walivaa nguo zenye maandishi ya WCB, waliandika maandishi haya kwenye Bajaj zao, walisokota nywele kama yeye na hata walipoongea walilamba midomo yao kama alivyofanya yeye.

Lawama zangu zote nikaamua kuzitupa kwa menejimenti yake, hapo nikimaanisha Babu Tale, Salam na Mkubwa Fela, kwamba hao ndiyo waliokuwa washauri na wasimamizi wakubwa wa Diamond Platnumz kama bidhaa, hivyo ndiyo waliomwambia fanya hiki na usifanye kile, bila shaka ndiyo waliopanga Diamond Platnumz afanye shoo nyingi zaidi nje ya nchi kuliko nchini Tanzania ambako hasa mashabiki wake wengi walikuwepo.

Kufuatia kujisikia kwangu hivyo kama mtakumbuka vizuri niliamua kuandika maelezo machache tu kwenye mtandao wa Facebook juu ya namna ambavyo mameneja wa Diamond walikuwa wakimpeleka msanii huyo shimoni, yalikuwa mawazo yangu, yangeweza kupingwa kwa hoja, lakini kilichofuatia baada ya hapo yalikuwa ni matusi kutoka kwa Babu Tale na mashabiki zao waliowaamuru wanitukane.

Nilitukanwa sana, nilidhalilishwa mno, wengi wenu mtakumbuka mpaka kipindi cha Shilawadu kilinirusha hewani, Babu Tale ‘akinichambua’ kuonesha kwamba mimi nilikuwa mtu mbaya niliyekuwa nikifanya kila kinachowezekana kumporomosha msanii Diamond, kwa kweli iliniuma, sababu niliandika kwa nia njema, inawezekana kuandika kwenye mtandao wa Facebook haikuifurahisha timu ya menejimenti ya Diamond. Lakini nifanye kitu gani wakati na mimi kuandika ndiyo kazi na kipaji changu kama ilivyo kwa Diamond kuimba? Muda wote wa mapambano hayo mtandaoni, Diamond Platnumz alikuwa kimya, hakutia neno, siamini kama alikuwa hajabariki kilichokuwa kikiendelea dhidi yangu.

Baada ya hapo hatukuwahi kuwasiliana tena na Diamond wala timu yake ya menejimenti, nilikuwa kimya nikifanya mambo yangu na wao wakafanya yao. Haukupita muda mrefu sana nikaanza kuona Diamond na timu yake wanafanya shoo nyumbani, wanatembelea Tandale na kuanza kutoa misaada, moyoni mwangu nilifahamu ingawa nilitukanwa, lakini nilichokisema kimesaidia.

Alhamisi wiki iliyopita nikiwa ofisini, simu yangu iliita, nilipoangalia kwenye kioo nilikuta namba nisiyoifahamu, hata hivyo, nikaamua kuipokea, masikio yangu yakakutana na sauti ngeni ambayo kwa kweli nilikuwa sijaisikia kwa muda mrefu, lafudhi ya Kikaguru au Kiluguru ikasikika; alikuwa ni Babu Tale.

Alinipa taarifa ya tamasha la hisani ambako Diamond alikuwa ameamua kulifanya Tandale, kwenye uwanja uleule ambao sisi na yeye tulifanya tamasha miaka mitatu iliyopita na aliniomba nihudhurie kwenda kuzungumza na vijana wa Tandale juu ya mafanikio na namna ya kutoka kwenye umaskini.

Sikuwa na uwezo wa kukataa kwa sababu kubwa mbili; moja, Diamond aliwahi kukubali mwaliko wangu na pili kazi iliyokuwa inakwenda kufanyika ndiyo ambayo mimi napenda kuifanya siku zote, kuwahamasisha watu kutoka kwenye umaskini! Nilikubali bila kusita kwamba ningekwenda kuifanya kazi hiyo kwa uaminifu.

Nilipowasili uwanjani siku ya Ijumaa, Agosti 5, sikuamini umati wenye maisha ya kawaida waliokuwa pale wakicheza muziki na kusikiliza hotuba, msanii Chid Benz alikuwa jukwaani akiwaeleza vijana juu ya kuachana na matumizi ya dawa za kulevya ambazo yeye alikuwa mhanga wake, watu walionekana kumsikiliza kwa makini.

Baada ya Chid Benz nilipanda jukwaani mimi mwenyewe na kuanza kuongea na vijana nikiwaleza juu ya umuhimu wa kutojidharau kwa sababu tu wamezaliwa familia maskini au kutokea mazingira ya watu maskini, kila mmoja wetu ana nafasi ya kufanya vizuri kama angefanya uamuzi sahihi maishani kwake kwa kujiepusha na tabia mbaya kisha kupambana usiku na mchana mpaka ndoto zitimie.

Wazungumzaji walikuwa wengi, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Paul Makonda alikuwepo, vivyohivyo Meya wa Kinondoni Mheshimiwa Benjamin Sitta, Msemaji wa Klabu ya Simba, Haji Manara kama nikitaja wachache tu, wote tulipomaliza kuzungumza ndiyo Diamond alipanda jukwaani na kuanza kuhutubia akielezea historia yake ya maisha na namna alivyofanya mpaka kufika mahali alipo.

Hakuwa mchoyo, hilo ndilo jambo linalotakiwa, aliwatia moyo wakazi wa Tandale alikotokea, mwisho alianza kutoa shukurani zake kwa kutoa bima za afya kwa watu 1,000 ambazo gharama yake ni zaidi ya shilingi milioni 30 za Kitanzania, akatoa Bajaj kwa mama mlemavu, bodaboda 20 kwa vijana wa maeneo hayo ili wapate kujiajiri.

Hakika kilikuwa ni kitendo cha ukarimu wa hali ya juu kabisa mimi kushuhudia kutoka kwa msanii wa Kitanzania, moyo wangu uliguswa mno, vinyweleo vilikuwa vimenisimama, moyoni mwangu nikasikia sauti ikiniambia ‘Toa na wewe’ ambayo naamini ilikuwa ni sauti ya Mungu.

Sikuwa na namna isipokuwa kutii, nikamwambia Babu Tale kwamba ningetoa bodaboda tatu pamoja na shilingi milioni moja kwa mama mlemavu aliyepewa Bajaj ili uwe mtaji wake wa kuanzia kuweka mafuta kwenye Bajaj hiyo wakati akifanya biashara yake ya kubeba abiria.

Sijawahi kuwa na msisimko kama nilioupata uwanjani hapo, kwa kweli jambo lililofanyika ni jema mno, Diamond Platnmuz pamoja na timu yake yote wamegusa sana moyo wangu, naamini pia moyo wa Mungu! Hiki ndicho nilichokuwa nikikipigia kelele huko nyuma mpaka nikaambulia matusi mengi mtandaoni, sasa kimetendeka, sina sababu ya kuongea chochote, Mungu aendelee kumbariki Diamond katika kazi zake.

Jambo moja kubwa ninaloliomba kwa Watanzania wote wala si wasanii peke yao, tuwe na tabia ya kukumbuka tulikotoka pale ambapo Mungu atatubariki kwa kitu chochote maishani mwetu, jambo hili litatuletea baraka zaidi katika mambo tunayoyafanya. Ninaposema kumbuka ulikotoka simaanishi tu kijijini kwenu, la hasha ila watu walio katika ngazi ya maisha ambayo wewe umeipitia.

Si lazima usubiri uwe na uwezo mkubwa kama Diamond Platnumz ndiyo usaidie watu, la hasha, bali ukiwa na afya wakumbuke wanaoumwa, ukiwa mezani unakula wakumbuke wenye njaa, ukiwa katika nchi yenye amani wakumbuke wanaoteseka katika vita, ukijihusisha na matatizo ya watu, Mungu atajihusisha na matatizo yako, kwa kitendo hiki alichokifanya Diamond kama kweli kimetokea moyoni na Mungu ameona, tutarajie makubwa sana katika maisha yake.
Asanteni sana kwa kunisoma,
Mungu awabariki.

Bongo5

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad