KIUNGO anayemudu kucheza nafasi ya ukabaji na uchezeshaji wa Yanga, Feisal Salum ‘Fei Toto’, ni kama amevuruga mipango ya Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mkongoman, Mwinyi Zahera kutokana na kuukosa mchezo ujao wa Ligi Kuu Bara.
Yanga katika mchezo ujao wa ligi, inatarajiwa kuvaana na Alliance ya jijini Mwanza Oktoba 20 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na Championi Jumatatu, mratibu wa timu hiyo, Hafidh Saleh alisema kuwa kiungo huyo atakosekana katika mchezo huo kutokana na kutumikia adhabu ya kadi tatu za njano ambazo alizipata katika michezo mitatu mfululizo ya ligi iliyopita.
Saleh alisema, kadi hizo alizipata kwenye mchezo dhidi ya Stand United, Singida United na Mbao FC.
Aliongeza kuwa, kocha msaidizi wa timu hiyo Mzambia, Mwinyi Zahera tayari ameanza mikakati ya kumpata mbadala wake atakayecheza nafasi hiyo katika mazoezi yanaondelea kabla ya kuwavaa Alliance.
“Siku zote mchezaji muhimu aliyepo katika kikosi cha kwanza akikosekana katika timu kwenye mchezo ujao kutokana na kadi au majeraha ni tatizo katika timu, ni lazima kocha atafute mbadala wake.
“Hivyo, kukosekana kwa Fei Toto kunaharibu mipango ya kocha licha ya kuwepo wachezaji wengine katika timu wanaomudu kucheza nafasi hiyo kama vile Raphael na Tshishimbi (Pappy Kabamba),” alisema Saleh.