Frederick Sumaye Amtahadharisha Katibu Mkuu wa CCM Dk Ally Bashiru Kuhusu Kauli yake


Dar es Salaam. Waziri mkuu mstaafu, Frederick Sumaye amesema kauli aliyoitoa Katibu Mkuu wa CCM, Dk Ally Bashiru ya kuwa vitendo vya rushwa na kutowajibika vinasababisha watu kupuuzia uchaguzi na kuuona kama ni maigizo ipo sahihi, lakini amemtahadharisha kuwa ajiandae kuchukiwa.

Wakati Sumaye akiyasema hayo, Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Bara), Magdalena Sakaya alisema kwa kauli hiyo, Dk Bashiru ameanza kuelewa na kuyaona yaliyoko ndani ya chama hicho tawala.

Wiki iliyopita, Dk Bashiru alitoa kauli hiyo mjini Morogoro katika Kongamano la Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (Mviwata) pale alipokuwa akizungumzia umuhimu wa wananchi kuiwajibisha Serikali.

Katika maelezo yake, Dk Bashiru alisema vitendo kama hivyo vikiwamo vya rushwa na kutowajibika, ndivyo vilisababisha nchi kupata Serikali iliyokosa uhalali wa kisiasa katika uchaguzi mkuu wa 2010 baada ya wapigakura chini ya asilimia 50 ya waliojiandikisha kujitokeza kupiga kura.

Akizungumza jana na Mwananchi, Sumaye ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema alisema anakubaliana na maelezo ya katibu mkuu huyo na kwamba, yeye aliwahi kuzungumzia kuhusu uchache wa kura ambao CCM ilipata mwaka 2010.

“Katika mikutano yangu mbalimbali na wanahabari niliwahi kusema kura ambazo CCM imepata katika uchaguzi wa 2010, chama hiki hakikuwa na uhalali wa kuwa chama tawala tena. Matokeo yake nikaanza kuchukiwa na kutopendwa ndani ya chama.

“Hii ndiyo dalili kubwa ninayoiona kwa Dk Bashiru ndani ya chama chake. CCM hawapendi kuambiwa ukweli kwa sababu wanaona watashindwa katika utekelezaji wa majukumu yao mbalimabli,” alisema Sumaye ambaye aliwahi kuwa Mbunge wa Hanang’.

Alisema alichokizungumza Dk Bashiru ni kujaribu kukitahadharisha chama chake ili kifanye kazi na kubadilisha misimamo yake kusudi kiendelee kuaminiwa na wananchi.

“Ni vema Dk Bashiru ameyasema haya. Lakini wangesema wapinzani tungeitwa wachochezi na kesho yake unaitwa na vyombo vya dola kuhojiwa,” alisema Sumaye.

Hata hivyo, alisema enzi za Jakaya Kikwete kulikuwa na unafuu kwa kuwa Serikali haikuwa ikiwakandamiza wapinzani na watu hawakwenda kupiga kura kwa sababu waliona hakuna maana licha ya aliouita ‘wizi’ wa CCM.

Alisema kulikuwa na mitazamo tofauti ikiwamo ya upinzani kutokuwa na uwezo wa kuchukua dola, lakini sasa hivi hali imebadilika watu wamejawa na hofu ya kupiga kura hasa kitendo cha matumizi ya vyombo vya dola kutumika katika vituo vya kupigia kura.

Naye Sakaya, ambaye ni Mbunge wa Kaliua (CUF) alisema alichokisema Dk Bashiru ndio uhalisia kwa sababu vitendo vya rushwa vimekithiri kwenye chaguzi mbalimbali na hali hiyo imechangia CCM kupoteza majimbo muhimu waliyowakuwa wameyashikilia katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.

“Kasahau kuongelea matumizi ya ubabe hasa vyombo vya dola kwenye uchaguzi.

“Ni wakati sasa kwa aliyoyasema yafanyiwe kazi ili tuwe na uchaguzi huru na haki. Sasa hivi wapigakura wanasita kupiga kura kwa sababu mshindi anajulikana kabla ya mchakato haujafanyika,” alisema Sakaya.

Mwananchi
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad