Godbless Lema ataka polisi wotoe picha za CCTV kutekwa kwa Mo

Godbless Lema ataka polisi wotoe picha za CCTV kutekwa kwa Mo
Mwanasiasa machachari wa upinzani Tanzania na Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani Godbless Lema amelitaka jeshi la polisi kutoa picha za CCTV kwa vyombo vya habari na mitandao ya kijamii ambazo zinaonyesha tukio la kutekwa kwa bilionea Mohamed Dewji.

Mwanasiasa huyo amesema kama serikali ipo tayari kupokea msaada kutoka kwa wananchi ili kufahamu mahali alipo Mo Dewji basi iachie picha hizo ili wananchi waweze kuwatambua watekaji na magari yaliyotumika.

"Baada ya kugundua kuwa waliomteka Mo ni wazungu wawili na wameonekana kwenye mkanda wa CCTV, na si polisi wanataka wananchi watoe ushirikiano? Chamuhimu una zitoa picha za video, hao wazungu tuwaone. Swali kwanini wanaficha hizo picha za CCTV? Kwanini hata kwa (Tundu) Lissu kamera ilichukuliwa?," amehoji Lema.

Zawadi nono kwa atakayewezesha kupatikana Mo Dewji
Maswali magumu kuhusu kutekwa kwa Mo
Tajiri mkubwa Afrika Mashariki Mo Dewji atekwa
Lema pia ameitaka serikali kukubali usaidizi katika upelelezi wa mkasa huo kutoka katika mashirika ya kijasusi ya nje ili kurudisha imani kwa wananchi na kufuta lawama kuwa inahusika na matukio ya kupotea kwa mwandishi Azory Gwanda, msaidizi za mwenyekiti wa Chadema Ben Saanane na pia kushambuliwa kwa risasi kwa mnadhimu mkuu wa upinzani bungeni Tundu Lissu.

"Ndio nasema serikali kujivua lawama kwenye maswala yote kwamba haihusiki ilete Scotland yard ama ilete mashirika mengine ya kiupelelezi duniani yaje yachunguze swala hili," Lema anaiambia BBC.

Hathivyo, serikali ya Tanzania kupitia Waziri wa Mambo ya Ndani Kangi Lugola imesema haitaomba usaidizi wa kiupelelezi juu ya mkasa wa kutoweka kwa Mo na mikasa mingine ikisema vyombo vya ulinzi vya ndani vinaweza kuitatua mikasa hiyo.

Mbunge huyo alipohojiwa juu ya uchunguzi wa namna gani aliofanya aliweka wazi kuwa ni uchunguzi wa kiintelijensia.

"Watu wengi wanadhani uchunguzi ni kwenda kuokota maganda ya risasi, hapana kuna uchunguzi wa kiintelijensia na uchunguzi wa kiupelelezi. Unaweza ukasimuliwa namna jambo lilivyotokea ukapata mashaka. Moja ya mashaka ni eneo ambalo Mo ametekwa lina ulinzi mkali na viongozi wengi wanakaa, ilikuwa ni rahisi atekewe kwake na siku zote huwa katika maeneo ya kijamii na hata gari huwa anaendesha mwenyewe. Na kwanini mpaka siku ya nne hawa watekaji hawajaomba kupewa pesa kama walitaka pesa?" anahoji Lema

Hata hivyo mwanasiasa huyo amefafanua kuwa kuzungumza kwake ni jukumu lake kama raia na kama waziri kivuli wa mambo ya ndani. Na amesisitiza kuwa kuzungumza kwake si kutokuwa na woga juu ya usalama wake.

"Maisha ya mtu yana thamani kuliko hofu niliyokuwa nayo. Ni jukumu letu kupiga kelele kuhakikisha haki inatendeka katika taifa hili. Sasa wanaweza wakanikamata, sijali. Sio kwamba sijali kwasababu siogopi mi napenda kulala na familia yangu napenda kulala na mke wangu. Wanaweza wakaniteka sijali, sijali kwasababu tumeogopa mpaka tafsiri ya uoga inaanza kupoteza maana," amesema Lema.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad