Haji Manara Awapa Somo TFF

Haji Manara Awapa Somo TFF
Baada ya kuwepo kwa tetesi za kusogezwa mbele mchezo wao wa Jumamosi dhidi ya African Lyon, Mkuu wa Idara ya Mawasiliano ya Simba, Haji Manara, amelishauri Shirikisho la Soka nchini (TFF) na Bodi ya Ligi kuacha mechi hiyo ichezwe ili kuepusha mlundikano wa viporo.

Manara, aliliambia Nipashe kuwa ushauri wake kama mdau wa soka mchezo huo uachwe kama ulivyopangwa kwa kwani kuuahirisha kunaweza kusababisha kuwapo kwa viporo vingi hasa kutokana na kuwapo kwa ratiba za michuano mbalimbali.

Alisema Simba itaanza kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika kuanzia Desemba na pia Januari itashiriki michuano ya Mapinduzi itakayosababisha mechi zao za ligi kusimama kwa kipindi hicho.

"Mimi nitoe ushauri tu kwa wenzetu wa TFF na Bodi ya Ligi..., msimu huu kila timu itacheza michezo 38, na kwa kufuata Kalenda ya FIFA ligi nyingi zinamalizika Mei mwakani, sasa tukianza kuweka viporo mapema nina wasiwasi baadaye huko mbele tutapata tabu kutokana na kubanwa na ratiba kutokana na Simba kushiriki mashindano mengine wakati huo huo hii ni Oktoba na hakuna hata timu iliyocheza michezo angalau 10 tu," alisema Manara.

Alisema anafahamu umuhimu wa Taifa Stars kuingia kambini kwa kuwa kama Mtanzania anapenda maendeleo ya timu hiyo.

"Kila Mtanzania anatamani kuona tuanafuzu fainali za Afrika, na mimi naunga mkono maandalizi ya timu yetu, lakini pia tuangalie namna ambayo wakati Taifa Stars ikiwa kwenye maandalizi yake, michezo ya Ligi Kuu iendelee, nashauri kama mdau wa soka na sio kauli ya klabu," alisema.

Simba ambayo Jumapili iliyopita ililazimishwa sare ya bila kufungana na watani zao, Yanga, Jumamosi itacheza na African Lyon kama ratiba hiyo haitapanguliwa na bodi ya ligi.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad