Khashoggi raia wa Saudia alikuwa mkosoaji kinara wa sera za Mwanamfalme Mohammed Bin Salman mara ya mwisho alionekana akiingia ndani ya ofisi za ubalozi mdogo wa Saudia jijini Istanbul, Uturuki Oktoba 2 na kuuawa akiwa ndani.
Awali Saudia walidai kuwa mwanahabari huyo ambaye alikuwa akiishi Marekani alitoka ndani ya ubalozi wake. Baada ya shinikizo wakasema kuwa aliuawa alipojaribu kupambana na baadaye wakakiri kuwa aliuawa katika opersheni isiyo rasmi na ambayo haikubarikiwa na Bin Salman.
Wengi wa washukiwa hao 15 waliingia Uturuki saa chache kabla ya Khashoggi kuingia kwenye ofisi za ubalozi kufuatilia nyaraka kuhusu ndoa yake na kuondoka Uturuki siku hiyo hiyo wakitumia ndege binafsi za kukodi.
Mamlaka za Uturuki zinaamini kuwa washukiwa hao ni maafisa wa uslama na majasusi wa serikali ya Saudia, tuhuma amabazo zinathibitika kwa vyanzo vya kiupelelezi vilivyowazi.
Washukiwa hao ni wafuatao;
Dkt Tubaigy ni daktari bingwa wa uchunguzi wa magonjwa ya binadamu ikiwemo uchunguzi wa sababu za vifo. Daktari huyo alipata shahada yake ya uzamivu kutoka Chuo Kikuu cha Glasgow, Uskochi na mwaka 2015 alifanya kazi kwa miezi mitatu katika kituo cha uchunguzi wa kitabibu cha Victorian nchini Australia.
Katika ukurasa wake wa Twitter, Tubaigy anajitambulisha kama mkuu wa Baraza la Wachunguzi wa Matibabu wa Saudia. Ukurasa huo unauhusiana na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Saudia.
Maafisa wa Uturuki wananadai kuwa Dkt Tubaigy alitua katika uwanja wa ndege wa Istanbul akiwa na msumeno. Daktari huyo aliingia Uturuki alfajiri ya Oktoba 2, na kufikia hoteli ya Movenpick iliyopo mita 500 kutoka katika ofisi za ubalozi wa Saudia. Aliondoka Uturuki siku hiyo hiyo saa 5 kasoro dakika nne usiku.
Inadaiwa sauti ya daktari huyo inasikika katika mkanda wa sauti ulionasa tukio la kuteswa kisha kuuawa kinyama kwa Khashoggi. Yanaiwa sauti ya mtu anayetambulika kama daktari ilikuwa ikiwaita wengine wasikilize muziki wakati akimkata Khasoggi vipande vipande.
Dkt Tubaigy hajazungumza kitu mpaka sasa, lakini bwana mmoja aliyejitambulisha kama mjomba wake ameandika katika mitandaoni kuwa daktari huyo hawezi kushiriki unyama kama huo.