Katika michuano ya AFCON, Cape Verde imeshiriki takribani mara nane, mara ya kwanza kwa nchi hiyo kushiriki michuano ya Afrika ni mwaka 1994 huku Taifa Stars ikiwa imeshiriki mara moja pekee mpaka sasa, ambapo ilikuwa ni mwaka 1980.
Taifa Stars na Cape Verde zimekutana mara mbili katika miaka ya karibuni, ambayo ni mwaka 2010 katika hatua ya makundi kuwania kufuzu michuano ya kombe la dunia iliyofanyika nchini Afrika Kusini.
Mchezo wa kwanza ambao ulifanyika jijini Dar es salaam, Taifa Stars iliibuka na ushindi wa mabao 3-1, mabao ya Taifa Stars yakifungwa na Athumani Idd 'Chuji' dakika ya 6', Jerson Tegete dakika ya 29' na Mrisho Ngassa katika dakika ya 75' huku bao pekee la Cape Verde likifungwa na Soares Silvino katika dakika ya 36' ya mchezo.
Kwenye mchezo wa marudiano, Taifa Stars ilifungwa bao 1-0 nchini Cape Verde na kushindwa kufuzu hatua inayofuata baada ya kumaliza nafasi ya tatu katika kundi lake, huku Cameroon na Cape Verde zikifanikiwa kusonga mbele.
Huu utakuwa mchezo wa tatu kuzikutanisha timu hizo katika mashindano ya kimataifa tangu mwaka 2010, ambapo kila timu ikijizatiti kutafuta alama tatu na hatimaye kuizidi ama kuisogelea Uganda ambayo inaongoza kundi mpaka sasa.