Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa imepanga kusoma hukumu ya kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu Tanzania, Abdul Nondo Novemba 5.
Nondo anakabiliwa na makosa mawili ya kusema uongo ambayo anadaiwa kuyatenda Machi 7, mwaka huu.
Akitaja tarehe ya hukumu hiyo, Hakimu wa Mahakama ya Hakimu mkazi Iringa, Liad Chamshama alisema jana Jumanne ilikuwa ni siku ya kuwasilisha hoja za mwisho za upande wa utetezi na upande Jamuhuri.
Upande wa mshtakiwa uliwakilishwa na Wakili Baruti baada ya mawakili Jebra Kambole na Chance Luwoga kuwa nje ya mkoa ambapo wakili huyo ameridhia kusomwa kwa hukumu ya mteja wao Novemba 5, mwaka huu.
Awali Abdul Nondo alifikishwa mahakamani hapo akikabiliwa na mashtaka mawili ambapo shitaka la kwanza lilikuwa ni kusema uwongo kwa njia ya mtandao wa kijamii wa WhatsApp kuwa yupo hatarini.
Shitaka la pili linalomkabili Abdul Nondo ni la kusema uongo kwa mtumishi wa umma ambaye ni askari wa Kituo cha Polisi Mafinga kuwa alitekwa na watu wasiofahamika Dar es salam na kutelekezwa Kiwanda cha Pareto Mafinga.
Pande zote mbili zimefunga kuleta ushahidi na mahakama imepanga tarehe hiyo kuwa siku itakayosomwa hukumu hiyo.