Maafisa wa uokozi wa Ufilipino wamesema kuna uwezekano kwamba abiria wote 189 pamoja na wafanyakazi wa ndege ya Indonesi ya Shirika la Lion iliyoanguka nchini humo wamefariki dunia.
Kwa mujibu wa DW Swahili, Maafisa wa uokozi wa Ufilipino wamesema kuna uwezekano kwamba abiria wote 189 pamoja na wafanyakazi wa ndege ya Indonesi ya Shirika la Lion iliyoanguka nchini humo wamefariki dunia. Tangazo hilo limetoklewa, baada ya kugunduliwa baadhi ya masalia ya miili ya binadamu ingawa waokozi wataendelea kupekua eneo hilo usiku mzima wa leo.
Ndege hiyo ya Boeing-737 MAX iliyofanyiwa ukaguzi mwezi mmoja tu uliopita, ilipotea kutoka kwenye rada dakika 13 baada ya kuondoka Jakarta, na kuanguka kwenye bahari ya Java, mara tu baada ya kuomba kurejea kwenye mji huo mkuu wa Indonesia. Kampuni ya Boeing yenye makao yake Marekani, imeeleza kusikitishwa na ajali hiyo.
Tovuti zinazotoa picha ya ndege hiyo, zilionyesha ikiwa inashika kasi na ghafla kuanza kushuka, dakika chache kabla ya kupotea, huku mamlaka zikisema washuhudiaji waliona ndege hiyo ikianguka kwenye maji.
Mapema, mkurugenzi wa kikosi cha uokozi Bambang Suryo Aji alisema wameona vipande vichache vya miili ya binaadamu tangu walipoanza operesheni hiyo majira ya asubuhi.
Alinukuliwa akisema “katika operesheni ya upekuzi iliyoanza kwenye eneo la juu ya maji tuliyoifanya tangu asubuhi hadi mchana wa leo, tumekuata vipande vichache vya sehemu ya miili ya binadamu. Ninadhani kwamba wengi wa wahanga bado wako ndani ya ndege kwa hiyo tunalazimika kufika haraka kwenye eneo ambapo ndege iliangukia, kwa sababu kuna uwezekano mkubwa wa kuzamia.”
Hata hivyo, alisema, bado ana hisia kwamba hakuna aliyenusurika kwa sababu masaa kadhaa yameshapita na kuna uwezekano mkubwa kwamba wote wamekufa.
Rais wa Indonesia, Joko Widodo amesema akiwa Bali anakohudhuria mkutano kwamba ameiagiza mamlaka inayohusika na usalama wa usafirishaji kufanya uchunguzi wa ajali hiyo. Amesema, kikosi cha uokozi kinafanya kila linalowezekana kuwapata wahanga na kuwataka Waindonesia kuwa watulivu.
Kamisheni ya Ulaya imesema kupitia msemaji wake Enrico Brivio kwamba haina tena mipango ya haraka wa kulizuia shirika la ndege la Lion Air la nchini Indonesia, baada ya ajali hiyo. Amesema wataangazia kwanza matokeo ya uchunguzi wa ajali hiyo.
Kiongozi wa kanisa Katoliki duniani, Papa Francis ametuma salamu zake za rambirambi kwa wahanga wa ajali hiyo ya ndege, iliayianguka dakika 13 mara baada ya kuruka na kusababisha vifo vya abiria na wafanyakazi hao, inayokadiriwa kuwa 189.
Waziri wa mambo ya nje wa Vatican kadinali Pietro Parolin amesema kupitia ujumbe aliwaandikia wawakilishi wa Vatican nchini Indonesia kwamba papa amewahahakikishia kuwa nao kwa sala wale wote waliokufa na wale wanaowaomboleza waliopoteza maisha kufuatia ajali hiyo.
Ndege hiyo ilikuwa inatokea Jakarta ikielekea jiji la Pangkal Pinang, eneo la watalii lililopo karibu na kisiwa cha Belitung.