Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro ameonesha kuchukizwa na maneno yaliyokuwa yakiandikwa na baadhi ya wanasiasa nchini ambao walikuwa wakikosoa moja ya taarifa yake kuhusiana na kubaini gari lililokuwa limemteka mfanyabiashara Mohammed Dewji kupitia mitandao ya kijamii.
Miongoni mwa wanasiasa ambao walikuwa msitari wa mbele kukosoa hatua hiyo ya IGP Simon Sirro ni Zitto Kabwe na Gobless Lema ambapo kamanda Sirro amesema hajui nia na malengo ya wanasiasa hao.
“Na niwaambie ukijenga uadui na jeshi la polisi na majeshi yetu, jana nilizungumza na waandishi nikiwa na uhakika lakini kuna watu wachache sijui nia yao ni nini kwenye matukio mengi yakifanyika wao ndio wanatufundisha wao ndio polisi ofisa, wao ndio wapelelezi.
“Niwaombe sana watu hawa wajitahidi kushirikiana na vyombo vya dola na kama wanatumika vibaya ili kuvikwamisha vyombo vya dola hatutawapa nafasi, na wananchi mnaona jana walianza kuzungumza kwenye mitandao lakini leo mmeona amepatikanana.” Amesema IGP Simon Sirro
Kupitia mitandao ya kijamii Mbunge wa Kigoma mjini na Waziri Kivuli wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi walionesha kutoridhika na baadhi ya taarifa za awali zilizotolewa na kamanda Sirro.
“Hawa Polisi @tanpol wanadhani kila mtanzania ni zwazwa anaweza kudanganywa danganywa tu. Taratibu za gari kupita mpakani zinatia mashaka makubwa kauli ya IGP.Polisi na vyombo vya usalama nchini hutumia plate number za Kigeni. Ile picha ya gari sio ya CCTV. Kamanda Sirro hapana.””Aliandika Zitto Kabwe
“IGP kwa hiyo kwenye mifumo ya cctv baada ya kurekodi huwa kuna majira ya hali ya hewa.”Aliandika Godbless Lema
Mapema leo alfajiri ya saa 11 kulianza kusambaa taarifa ya kupatikana kwa mfanyabiashara Mohammed Dewji ambaye inasadikika watu waliomteka walimtelekeza kwenye eneo la Gymkhana jijini Dar es salaam.