Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Simon Sirro amewataka wafanyabiashara na watu wenye uwezo kifedha kuwa na silaha ili kujilinda kwa kile alichodai kuwa dunia imebadilika.
Sirro ametoa kauli hiyo katika mkutano wake na wanahabari leo, Oktoba 19, wakati akizungumzia sakata la kutekwa kwa mfanyabishara, Mohammed Dewji, ambapo amesema kuwa taarifa zinazosambaa mitandaoni ziwe za kusaidia na kujenga na sio za kuumiza upande mmoja kwakuwa lengo ni moja kuhakikisha anapatikana mfanyabishara huyo.
"Niwaombe ndugu zangu wenye uwezo wa kifedha ni vizuri kuwa na silaha kujilinda, dunia imebadilika, MO ana silaha lakini siku ile hakubeba silaha, anakuwa na dereva lakini siku ile hakuwa na dereva", amesema IGP Sirro.
Sirro ameongeza kuwa, "Tuliokota risasi katika eneo lilipofanyika tukio la utekwaji wa Mo Dewji tumekwenda kuzifanyia uchunguzi kwenye maabara yetu, ina ukubwa wa milimita 9".
IGP Sirro pia ametoa takwimu za mwezi Machi hadi Septemba 2018 za jeshi hilo katika oparesheni ya kupingana na matukio ya kihalifu, akisema kuwa Jeshi hilo limekamata silaha 190, zikiwemo K47 10 pamoja na risai 235 za aina mbalimbali.