Baada ya kusambaa kwa taarifa zilizodai kuwa Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari katimkia Chama cha Mapinduzi (CCM) na kujiuzulu nafasi yake ya Ubunge na uanachama wa CHADEMA, ofisi ya mbunge huyo imekanusha taarifa hiyo.
Kupitia taarifa iliyotolewa na Katibu wa ofisi ya Mbunge huyo leo Oktoba 24, Julius Ayo imesema kuwa, Nassari hayupo nchini na amekwenda nchini Marekani kwa shughuli za kikazi kuhusiana na jimbo lake.
"Habari zinazo sambaa mitandaoni tangu juzi kuhusu Mbunge wa jimbo la Arumeru Mashariki kujivua Ubunge na Kujiunga na CCM siyo za kweli, puuzeni habari zinazo sambazwa na wajinga wachache", amesema Julius.
Kupitia mitandao ya kijamii zilisambaa taarifa zilizodai kuwa Nassari amejiunga na CCM ili kuunga mkono jududi za Rais Magufuli na kujivua nafasi yake ya Ubunge kupitia CHADEMA.
Mpaka sasa jumla ya Wabunge tisa wa upinzani wamejiunga na CCM, ambao ni Maulid Mtulia (Kinondoni), Godwin Mollel (Siha), Julius Kalanga (Monduli), Mwita Waitara (Ukonga) ambapo wanne hao walipojiunga CCM walipitishwa kuwania ubunge na kuibuka na ushindi.
Wengine ni Zuberi Kuchauka (Liwale) ambaye pia ameshinda ubunge katika jimbo hilo kwenye uchaguzi uliokaofanyika Oktoba 13, 2018, huku ambao wanasubiri uchaguzi wa marudio kwa sasa ni aliyekuwa Mbunge wa Ukerewe (CHADEMA) Joseph Mkundi, Mbunge wa Babati (CHADEMA) Pauline Gekul, James Ole Millya (CHADEMA) Simanjiro na Marwa Chacha aliyekuwa mbunge wa Serengeti kwa tiketi ya CHADEMA.
Joshua Nassari Azungumzia Tetesi za Kuitosa CHADEMA na Kuhamia CCM
0
October 24, 2018
Tags