UNAWEZA kusema mambo ni mazuri kwa upande wa kipa wa Yanga, Beno Kakolanya ambaye mpaka sasa anaonekana kumkimbiza kipa wa Simba, Aisha Manula kutokana na kuwa na takwimu bora kwenye ligi.
Kipa huyo wa Yanga amecheza jumla ya dakika 329 na kuruhusu bao moja pekee ambalo alifungwa katika mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar ambao walishinda mabao 2-1.
Yanga imefanikiwa kucheza mechi sita na aliweza kudaka mechi nne dhidi ya Simba (0-0), Singida United (2-0), Mtibwa Sugar (2-1) na ule dhidi ya Mbao FC, ambao alidaka mpaka dakika 59 alitoka baada ya kuumia na nafasi yake kuchukuliwa na Klaus Kindoki.
Kipa wa Simba, Aisha Manula
Timu hiyo imecheza mechi sita na kufunga mabao 11 na kuruhusu mabao manne moja la Beno na matatu ya Kindoki.
Kwa upande wa Manula ambaye msimu uliopita ndiyo aliibuka kuwa kipa bora kwa mara ya pili mfululizo kwenye kikosi chake wamecheza mechi saba na zote amedaka mwenyewe.
Katika mechi hizo saba ameruhusu mabao matatu, ambayo alifungwa kwenye mchezo wao dhidi ya Mbao FC (0-1), Mwadui FC (1-3) na African Lyon (2-1).
Mechi nyingine ambazo Simba imecheza ni dhidi ya Tanzania Prisons (1-0), Mbeya City (2-0) Yanga (0-0) na Ndanda FC (0-0).
Msimu uliopita ligi ilipomalizika Manula katika mechi 29 aliweza kuruhusu mabao 14 ambayo ndiyo yalikuwa machache kwenye ligi huku Kakolanya msimu uliopita hakuwa na nafasi ndani ya kikosi chake.
Ukiachana na michezo ya ligi, Manula aliruhusu pia bao moja kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii, wakati Simba ilipovaana na Mtibwa Sugar na kuibuka na ushindi wa bao 2-1.
Hata hivyo, Manula pia amesharuhusu mabao matatu kwenye michezo miwili ya timu ya Taifa, huku Kakolanya akikaa nje, hii inaonyesha kuwa kipa huyo wa zamani wa Azam amesharuhusu mabao saba kwa msimu huu hadi sasa.