Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola amewataka makamanda wa polisi wa mikoa kujitathmini kama wanatosha katika nafasi hizo, vinginevyo wajiandae kuziachia.
Lugola alitoa kauli hiyo jana alipofanya ziara ya kushtukiza katika kituo kikuu cha polisi jijini Dodoma, ambapo pamoja na mambo mengine alisema baadhi ya makamanda hawajaanza kutekeleza maagizo yake kwa madai kuwa yamekuwa yakitolewa kisiasa zaidi.
“Wakuu wote wa vyombo vya ulinzi na usalama ikiwa ni pamoja na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) wawe mguu sawa, maana hawajui siku wala saa nitakapoibuka kwenye vituo na mikoa yao ili kuangalia maagizo yangu kama yanatekelezwa au la, wengi wataondoka na kuwapisha wenye weledi na uwezo wa kufanya kazi,” alisema Lugola.
Alisema atamuandikia barua Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro kuhusiana na maagizo anayoyatoa kwamba lazima yatekelezwe na makamanda wa mikoa, lakini atakayeshindwa atalazimika kuwapisha wenzake.
Waziri Lugola alirudia kauli yake kuhusu makosa yenye dhamana kwamba lazima watu wapewe dhamana iwe sikukuu, usiku au siku za mwishoni mwa wiki na kuwa Mtanzania yeyote ana haki ya kumwekea dhamana mtuhumiwa.
“Inspekta Jenerali wa Polisi namuelekeza kwamba kila raia wa nchi hii awe mfugaji, mvuvi, mkulima au mfanyabiashara anayo haki ya kumdhamini Mtanzania mwenzake,” alisema.
Lugola alisema, “Kinachotakiwa ni kutimiza vigezo vya huyo anayemdhamini kama anafahamika, anatambulika na ataweza kumleta huyo aliyemdhamini kwenye kituo cha polisi siku ambayo ameelekezwa kwenye hati yake ya dhamana.”
Akizungumza katika ziara hiyo, kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto aliahidi kuzifanyia kazi dosari zilizojitokeza ikiwemo ya kutotolewa dhamana kwa watu wanaostahili, kukosekana kwa taarifa za watuhumiwa na kukosekana kwa kibali cha kuhalalisha kuuzwa kwa pikipiki zilizokamatwa na kukosekana wamiliki wake.
Kangi Lugola Atoa Maagizo Mazito Baada Ya Kubaini Makanda wa Polisi Hawatekelezi Maagizo Yake Anayotoa
0
October 29, 2018
Tags