Si jambo la kushangaza kusikia Kanye West mmoja kati ya wasanii maarufu zaidi duniani katika miondoko ya kufoka foka amekutana na Rais wa Marekani Donald Trump.
Kwa muda mrefu sasa amekuwa akionyesha hisia zake wazi wazi za kumsifu Trump kupitia ukurasa wake wa Twitter na mahojiano mbali mbali.
Hata hivyo amekuwa akiwakosoa wanaomkemea kwa kuwataka wamwache awe na uhuru wa mawazo yake.
Kanye West alialikwa katika ikulu ya Marekani kwa ajili ya chakula cha mchana kujadili masuala mbalimbali ikiwemo mageuzi katika magereza, ajira na masuala ya wamarekani weusi.
Ni mjadala uliojaa vioja vingi kutokana na ukweli kwamba Trump na Kanye wote ni wazungumzaji sana na hutumia zaidi mtandao kuweka wazi hisia zao.
Katika majadiliano hayo yaliyolenga siasa, mageuzi na uzalishaji, West alinukuliwa akisema "wamejaribu kunitisha, marafiki zangu kuhusu kuvaa hii kofia, lakini hii kofia inanipa nguvu".
Kanye alienda mbali zaidi na kusema kofia hiyo iliyoandikwa "Make America great again" maneno yanayowakilisha kauli mbiu ya utawala wa donald Trump inamfanya anajionea fahari sana na anajiona kama Superman na aliongeza kuwa Trump ametengeneza kofia shujaa kwa ajili yake.
Hata hivyo alitoa hoja zake mbali mbali ikiwemo kwa sasa shule zina upweke zaidi na sio kama simu
"Mara nyingine watu wanasema mtoto huyu hana uwezo wa kusikiliza kwa makini, Hauna huo ugonjwa, shule imejaa upweke, sio ya kufurahisha kama hii," anasema Kanye huku akionyesha simu yake ya mkononi.
Pia alimtaka Rais Trump ajenge viwanda katika mji alipozaliwa wa Chicago na alimpongeza Donald kwa kufanikiwa kusimamisha vita na Korea kaskazini.
Kanye West Adai Kofia ya Trump Imempa Nguvu za Superman
0
October 12, 2018
Tags