Katibu Mkuu CCM Dk. Bashiru: Serikali ya Mwaka 2010 Ilikosa Uhalali Kisiasa

Katibu Mkuu CCM Dk. Bashiru: Serikali ya Mwaka 2010 Ilikosa Uhalali Kisiasa
Katibu  Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally amesema kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, mwaka 2010 nchi ilipata Serikali ambayo haikuwa na uhalali wa kisiasa.

Dk. Bashiru aliyasema hayo jana mjini Morogoro, alipokuwa akitoa mada katika Kongamano la Mtandao wa Vikundi vya Wakulima (Mviwata) lililofanyika Ukumbi wa Chuo Kikuu cha Kiislamu Morogoro.

Alisema Serikali hiyo ilipatikana kwa sababu zaidi ya asilimia 50 ya wapigakura waliojiandikisha kupiga kura hawakujitokeza siku ya uchaguzi.

Katika uchaguzi wa mwaka 2010 ambao Jakaya Kikwete alichanguliwa kuongoza Serikali kwa awamu ya pili, wapigakura waliojiandikisha walikuwa 20,137,303 lakini waliojitokeza kupiga kura walikuwa 8,626,283 sawa na asilimia 42.84.

Jana akizungumza mjini hapa, Dk. Bashiru alisema; “jambo la nne ninalotaka kuzungumza ni uwajibikaji, mna nafasi gani ya kusimamia Serikali ili iwe upande wenu, kwa sababu ukweli ni kwamba mamlaka ya Serikali yako mikononi mwa umma na umma ni walio wengi ambao ni ninyi.

“Na vyeo vyote vilivyopo Serikali ni mali yenu, isipokuwa kuna mchakato wa usimamizi wa vyeo vyenu kupitia Serikali na moja ya michakato ni uchaguzi, hebu tujiulize tabia yenu na mwenendo wenu wakati wa uchaguzi ikoje?

“Tuambizane ukweli, mkishapewa kofia na T-shirt (fulana), alafu nyimbo zikaanza kupigwa za ‘mbele kwa mbele’, huwa mnapata nafasi za kuhoji sifa za mnayetaka kumchagua?

“Je, sifa ya chama mnachotaka kukichagua kinachopiga ‘mbele kwa mbele’ unaijua?

“Kwa hiyo eneo jingine muhimu kwa nafasi yenu ni kuwa sehemu ya mchakato ya kuwajibisha wote wenye vyeo vyenu. Kwahiyo msichague kiongozi kwa T-shirt, kwa kofia, kwa ubwabwa, kwa pesa.

“Kwa kufanya hivyo mnatengeneza watu watakaokuja kuwaonea, kwa sababu dhuluma zote na uonevu hazifanywi na wakoloni, zinafanywa na wale mliowachagua nyie wenyewe. Au wale walioteuliwa na wale mliowachagua.

“Sasa watu ambao ni wajanja, mimi naweza kusema wapigakura wa Tanzania ambao wamefikia hatua ya kudharau uchaguzi, wanakaa nyumbani (siku ya uchaguzi) kwa sababu wanaona ni kama kituko, ni mchezo wa kuigiza.

“Na ndiyo maana leo kupata watu kuhudhuria kupiga kura imekuwa shida, kote tunakoshinda ni chini ya asilimia 30, chini ya asilimia 40, hakuna mahala ambako wapigakura wamejitokeza kwa zaidi ya asilimia 50.

“Na mwaka 2010 ilitia fora, watu wengi walijiandikisha zaidi ya asilimia 100, kumbe walikuwa wanataka kile kipatarata (kitambulisho cha mpigakura) kwa sababu kinatumika kwenda polisi kudhamini, unajitambulisha, walipokipata wakaingia mitini.

“Kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hii, tulipata Serikali ambayo haikuwa na uhalali wa kiasiasa kwa sababu wapiga kura wengi zaidi ya asilimia 50 walibaki nyumbani na tatizo hili halijaisha, lakini mwanasiasa akishashinda anasema ushindi ni ushindi tu hata kama ni kwa kura moja.

“Hajali kwamba ushindi ule unatakiwa uwe na uhalali, tulifika mahala ambapo ikifika wakati wa uchaguzi wagombea wanauza nyumba, wanakopa, wanaitisha mikutano ya kuchangisha, usipomchangia mkali utafikiri anakwenda hospitali kutibiwa.

“Akishazikusanya zile fedha anaenda kuwanunua mawakala na mawakala wanawanunua wapigakura, msimu wa uchaguzi unakuwa msimu wa rushwa ya uchaguzi, ninachowaomba nafasi yenu ni kubomoa na kuharibu soko la kura.”

Dk. Bashiru alisema kwa sababu kama CCM itakuwa imejipanga, mipango mizuri ya kuhudumia umma ipo, wananchi wanaona shule, hospitali hakuna haja ya kwenda kuhonga.

“Ukiona mtu anakuhonga hana sifa, na ndani ya CCM tumeshasema itakuwa sababu ya kutoteua mtu huyo hata kama atakuwa ameshinda kura za maoni.

“Kwa sababu bila kuwa na mfumo wa kuwapata viongozi, na nasikia sasa hivi rushwa imeenda mpaka kwa wenyeviti wa vijiji, kitu ambacho ni hatari, kwa sababu mwenyekiti wa kijiji anasimamia mazingira na wananchi wake, anasimamia migogoro na wananchi wake, anasimamia haki na wananchi wake, akianza kununua uongozi atauza ardhi.

“Kwahiyo mambo haya manne kwangu mimi naona ni muhimu sana, ili uweze kupata nafasi katika uchumi wa taifa hili, uwezo wenu wa kutambua mambo, kutambua kwamba benki ya ardhi ni wizi, kwamba bodi za mazao ni wizi na mimi nashangaa mpaka leo Bodi ya Kahawa ipo,” alisema.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad