Khamis Kagasheki "Kauli ya Bashiru Ally Ningeitoa Mimi Nisingebaki Salama"


Waziri wa zamani wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki. 

Dar es Salaam. Waziri wa zamani wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki amesema asingebaki salama kama angetoa kauli kama ya Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally kuwa vitendo vya rushwa na kutowajibika vinasababisha wananchi kupuuza uchaguzi na kuona kama maigizo.

Licha ya kueleza hayo, Balozi Kagasheki amesema anakubaliana na kilichoelezwa na katibu mkuu huyo wa chama tawala.

Dk Bashiru alitoa kauli hiyo mjini Morogoro katika Kongamano la Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (Mviwata) kuhusu umuhimu wa wananchi kuiwajibisha Serikali.

Katika maelezo yake, Dk Bashiru alisema vitendo hivyo vya rushwa na kutowajibika vilisababisha nchi kupata Serikali iliyokosa uhalali wa kisiasa mwaka 2010 baada ya wapigakura chini ya asilimia 50 ya waliojiandikisha kujitokeza kupiga kura.

Balozi Kagasheki, ambaye alijiuzulu uwaziri wa Maliasili na Utalii Desemba 2013 baada ya Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira kutoa ripoti iliyoonyesha ukiukwaji wa haki za binadamu wakati wa utekelezaji wa Oparesheni Tokomeza iliyolenga kutokeza ujangili, alisema hayo katika akaunti yake ya mtandao wa Twitter.

“Nimeyaelewa vizuri sana maelezo ya Dk Bashiru kuhusu upigaji kura wa wananchi, uhalali wa Serikali, matamshi ya viongozi,’ ameandika Balozi Kagasheki.

“Anao mtazamo mpana kuhusu chama chetu na Taifa letu. Maneno yaleyale ningeyasema mimi, naamini baadhi ya wanachama wenzangu wasingeniacha salama.”

Alipoulizwa na Mwananchi kuhusu maana ya kauli hiyo kuwa wanachama wenzake wasingemuacha salama, Balozi Kagasheki alisema hawezi kuongeza neno na kwamba ujumbe huo unatosha.

Katika hotuba yake, Dk Bashiru alitumia hadi mifano inayoihusu CCM, akisema wananchi huwa hata hawaulizi habari za mgombea au chama kinachowapigia wimbo wa “Mbele kwa Mbele” wakati wa kampeni na kugawa fulana na kofia ili wampigie mgombea au chama hicho.

Wimbo huo wa “Mbele kwa Mbele” hutumiwa na CCM katika mikutano yake mbalimbali, ikiwamo ya kampeni za uchaguzi.

Alisema hata “ushindi wetu”, akimaanisha wa CCM, umekuwa ukipatikana katika idadi ya wanaojitokeza isiyozidi asilimia 50.

Lakini, wakati Kagasheki akieleza hayo, katibu mkuu wa zamani wa CCM, Luteni Yusuf Makamba amesema kauli iliyotolewa na Dk Bashiru ni sahihi.

Kama ilivyokuwa kwa Balozi Kagasheki, katibu huyo wa zamani pia hakutaka kuingia kwa undani kufafanua kauli yake, akisema si sahihi kuchambua kauli ya kiongozi wake aliye madarakani.

“Mimi nilikuwa katibu mkuu wa chama na kwa sasa Dk Bashiru ndiyo bosi wetu. Siwezi kuongezea kitu. Alichosema ni sahihi, lakini siwezi kuongezea,” alisema Makamba.

“Ni sawa na kuongezea kauli aliyotoa Rais. Akishasema amesema. Wewe andika hivi ‘alipoulizwa, Mzee Makamba alisema swadakta’,” alisema.

Makamba aliteuliwa kuwa katibu mkuu wa CCM mwaka 2006 akirithi mikoba ya Philip Mangula ambaye kwa sasa ni makamu mwenyekiti wa chama hicho upande wa Bara.

Makamba alishika nafasi hiyo kwa miaka mitano na mwaka 2011 nafasi yake ilichukuliwa na Wilson Mukama, wakati wa mkakati wa kukisafisha chama uliopewa jina la “Kujivua gamba”.

Aidha, kada wa zamani wa CCM, Njelu Kasaka akizungumzia kauli ya Dk Bashiru alisema sababu kadhaa za kupungua kwa hamasa ya wapigakura ni kuchoshwa na uwingi wa chaguzi.

“Kwanza kuna kitu kinaitwa election fatigue (uchovu unaotokana na uchaguzi). Watu wameshazoea kuwa uchaguzi ni baada ya miaka mitano, lakini (hivi sasa) kila baada ya mwezi uchaguzi,” alisema.

“Sababu ya pili ni sababu zenyewe za uchaguzi. Kama watu walishachagua chama na mtu waliyemuamini wanasubiri tena miaka mitano au labda kitokee kifo. Lakini mtu anahama chama hiki na kwenda huku na kupitishwa kugombea, wapigakura wanaona ni usaliti.”

Pia alisema wananchi wanaona matokeo ya chaguzi hizo yanakibeba chama tawala.

“Watu wamechoka kwa sababu matokeo yanajulikana wazi kuwa atashinda mgombea gani. Usiwadharau wapigakura, hata kama hawakusoma wana hekima. Wanajua kabisa hata wakipiga kura matokeo yatakuwaje,” alisema.

“CCM wasidharau hali hii kwa kuwa itaathiri uchaguzi wa 2020. Uchaguzi ni sawa na mechi ya mpira na ili watu wengi waje kushangilia ni lazima kuwe na timu zenye upinzani na wasijue matokeo. Lakini kama wanajua kabisa timu fulani itashinda, hawawezi kuja kuangalia.”

Kasaka aliwataka viongozi wa Serikali kutowaamulia wapigakura cha kufanya na badala yake wawaache wanasiasa kushindana.

Pia, alimtaka Dk Bashiru kuchukua hatua kurekebisha hali hiyo.

Maelezo ya Kasaka yanalingana na ya Profesa Gaudence Mpangala aliyesema wananchi wanaona wanachezewa kutokana na wanaojivua uongozi kupitishwa kugombea tena.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad