Tukio hilo la aina yake limetokea Oktoba 3 mwaka huu, majira ya saa 3:00 katika Kijiji cha Kihumbu, Kata ya Hunyari, wilayani Bunda na kusababisha bwana harusi mtarajiwa huyo kuambulia kipigo na kukosa mke, kabla ya kuangukia mikononi mwa polisi.
Tukio hilo la kufedhehesha lilimkumba Marwa baada ya Chacha Nyamahi, mkazi wa Kijiji cha Makundusi, Kata ya Nata wilayani Serengeti kuuarifu uongozi wa Kijiji cha Kihumbu kuwa anatafuta mifugo yake (ng’ombe) 48 ambao waliibwa wakiwa malishoni Oktoba 2, mwaka huu.
Nyamahi alisema siku hiyo, akiwa safarini majira ya alfajiri, kijana mmoja alifika nyumbani kwake na kumkuta mkewe pamoja na mchungaji wa ng’ombe zake zipatazo 300 akawaambia kuwa ameagizwa na baba mwenye mji kwenda kusaidiana na mchungaji huyo kuchunga kwa kuwa ng’ombe ni wengi.
“Kwa kuwa ilikuwa ni asubuhi sana muda wa kupeleka ng’ombe ulipofika alimwambia mchungaji waende wakachunge wote. Waliondoka wakamuacha mke wangu nyumbani na hapo nina eneo kubwa kwa ajili ya kuchungia, walipofika mbele kidogo akamwambia mchungaji wangu rudia sabuni nyumbani tuje tuoge hapa kisimani mimi nitaangalia hawa ng’ombe, mchungaji wangu aliporudi nyumbani kufuata sabuni yeye akaswaga baadhi ya ng’ombe akaondoka nao,” alisema Chacha.
Ilidaiwa kuwa, mtuhumiwa huyo aliwaswaga ng’ombe wengi lakini kwa kuwa alikuwa peke yake wengine walirudi nyumbani na mchungaji aliporejea kufuata sabuni hakumkuta yule mtuhumiwa na baadhi ya ng’ombe wametoweka.
Baada ya Nyamahi kurudi kutoka safarini ndipo walianza kuwatafuta na walifika kijijini hapo na kutoa taarifa kwa uongozi ambapo waliwaambia kuwa kuna ng’ombe wenye alama alizozisema wametolewa mahari siku hiyo.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kihumbu, Alphonce Kiruki, aliliambia gazeti hili kuwa walimhoji mlalamikaji kama ng’ombe wake walikuwa na alama akasema wanazo wameandikwa herufi NY, walipowakagua wakakuta alama hizo ndipo viongozi wakashauriana wapige yowe kwa sababu ng’ombe waliotolewa mahari mchana kwa Nera Buyunge (shemeji wa bibi harusi) walikuwa na alama hizo.
“Kama unavyoona ndugu usiku huu baada ya kusikia yowe na kweli tumekuta ng’ombe hawa 18 wenye alama aliyosema huyu mlalamikaji na ng’ombe hawa tuliwaona mchana tulipokuja kwenye sherehe ya kupokea mahari kwenye familia hii.
“Tumewakamata vijana wawili (bwana harusi na mwenzake) na baba mwenye mji huu amekimbia. Vijana hawa walikuja na bwana harusi wakiwa wanne, wawili nao walipofungiwa ndani ya nyumba hii ya baba mwenye mji, wamepita juu ya dari na kukimbia,” alisema Kiruki.
Bwana harusi huyo mtarajiwa James Marwa, alipoulizwa na uongozi wa kijiji aliwapata wapi ng’ombe hao alisema kuwa aliwanunua kwa mchungaji aliyekuwa malishoni kwa sh. milioni 1.8, kila mmoja akiwa na thamani ya sh. 100,000.
Naye bibi harusi mtarajiwa (Prisca) aliliambia gazeti hili kwamba hakujua kama mwanaume huyo ni mwizi kwani kabla ya kulipa mahari alimwomba yeye pamoja na wifi yake watangulie kwa dada yake ili yeye aende mnadani kununua ng’ombe wa kuwatoa mahari.
“Kweli juzi alikuja na ng’ombe nikajua amewanunua mnadani na muda wa wiki tatu nilizoishi naye alikuwa akinieleza kuwa ni mfanyabiashara wa ng’ombe na hivyo nikamuamini, kwa kweli amenihuzunisha sana na kwa sasa simuhitaji tena,” alisema Prisca.
Dada wa bibi harusi mtarajiwa, Tabu Edward, alisema walipokea ng’ombe hao ikiwa ni mahari kwa ajili ya mdogo wake lakini hawakujua kuwa bwana harusi aliwaiba kwa kuwa siku zote aliwaambia kuwa anafanya biashara ya kuuza ng’ombe minadani na pia ni mkulima na mfugaji.
“Alikuja kumchumbia mdogo wangu Prisca mwanzoni mwa mwezi wa tisa mwaka huu hapa kwangu maana nilikuwa naishi naye mdogo wangu. Huyo kijana aliletwa na ndugu zetu wanaoishi wilayani Serengeti ambapo niliwauliza vipi tabia ya huyu kijana, wakasema ana tabia nzuri lakini ndipo yakatokea yaliyotokea baadaye,” alisema Tabu.
Tabu alisema kabla ya kupeleka mahari bwana harusi huyo alimwambia bibi harusi mtarajiwa pamoja na wifi yake yaani dada, yake watatangulia kwenda Kihumbu kwa ajili ya kufanya maandalizi ya sherehe na walipofika walienda wakakopa vinywaji, mbuzi watatu kwa ajili ya kufanya kitoweo, mchele, sukari na walikodi muziki vyote vikiwa na thamani ya Sh.700,000.
“Hapa nilipo sijui nitatoa wapi fedha za kulipa madeni hayo maana bwana harusi alisema tukope akija atalipa jana, (Oktoba 2) ambapo majira ya saa 2:05 usiku alikuja na vijana wenzie wanne na ng’ombe 18. Asubuhi kulipokucha alitoa ng’ombe 10, ng’ombe wanane waliobaki alidai ni wa biashara na hivyo tukabaki tunamdai ng’ombe watano na kuahidi kumalizia Desemba, mwaka huu,” alieleza Tabu.
Kwa mujibu wa Tabu, ng’ombe waliobaki alisema anakwenda kuwauza mnadani ili alipe deni la shilingi 700,000 iliyotumika kwenye sherehe na wakati wakiendelea kuburudika ndipo yowe ilipigwa wanakijiji wakavamia nyumbani hapo wakiwa na mzee aliyedai kuibiwa ng’ombe wake.
Mtendaji wa Kijiji cha Kihumbu, Deborah Wambura, alithibitisha kukamatwa kwa bwana harusi huyo mtarajiwa huku mwingine aliyekuwa naye akifanikiwa kuwakimbia wananchi wakiwa njiani kuelekea ofisini kwa mtendaji huyo siku huo.
“Hapa ofisini kwangu askari polisi wa kutoka Wilayani Bunda wamemchukua mtuhumiwa mmoja ambaye ni bwana harusi tu baada ya mwenzake kukimbia. Kwa kweli kitendo hiki si kizuri hata kidogo nawasihi vijana wanapotaka kuoa watafute mahari halali,” alisema mtendaji. Alipotafutwa Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Mara, SACP Juma Ndaki ili kuzungumzia tukio hilo, simu yake iliita muda mrefu bila kupokelewa.