Kinachowavuta Wanaume Kwenye Maumbo ya Wanawake


HAYA ni mambo yanayoakisi chura, ni mnyama anayeishi majini na nchi kavu, ukiwa jirani na dimbwi lililotuama maji, basi ifikapo jioni mara nyingi utasikia muziki wa vyura, ukitoa milio tofauti tena wakishindana usiku kucha kuimba nyimbo zisizokwisha.

Ni milio yenye mirindimo ya sauti inayosafiri mbali, tena huwa kero kwa jirani zao kama wakati huo wanahitaji utulivu na kupumzisha akili na mwili.

Mwaka 2016 msanii wa Bongo fleva Snura Mushi, alitunga wimbo alioupachika jina chura ambao ulipata umaarufu na kupepea kwenye vyombo vya habari.

Jina la chura lilifanya mapinduzi makubwa kwenye matumizi ya Kiswahili kwa kutuongezea msamiati chura wenye maana tofauti na ile iliyozoeleka miaka mingi. Pia kwenye Kiswahili cha mtaani kilipatikana faida ya kuongezeka kwa msamiati zaidi.

Ukirudi kwenye Kiswahili sanifu, chura ina maana tofauti na maana ya msanii Snura. Huyu ni mnyama mdogo mwenye miguu minne, asiye na mkia, anayerukaruka sana tena anayeishi majini na nchi kavu.

Ila chura wa Snura hakuwa mnyama wala hana sifa za kuishi majini bali ni sifa iliyotumika ikiwa imefichwa ili kuelezea sifa maridhawa juu ya maumbile ya mwanamke akimaanisha makalio.

Hapa chura ametumika kama kivumishi cha sifa na kwenye hilo Snura alifanikiwa katika ubunifu kwani leo wanawake kwa wanaume wote wanatumia neno chura kumsifia mwanamke mwenye makalio makubwa.

Lakini Snura alikumbana na rungu kutoka Baraza la Sanaa la Taifa mnamo Mei 4, 2016 ambapo vyombo mbalimbali vya habari vilitoa taarifa ya kufungiwa wimbo wa chura. Silaumu wala kuingilia kazi za mamlaka ya baraza, naamini lilitimiza majukumu yake kwa mujibu wa taratibu na sharia za nchi.

Kumbe Chura aliyezungumziwa na Snura siyo yule anayepiga kelele kwenye madimbwi ya maji wakati wa jioni, wala siyo wa maabara anayepasuliwa kwa ajili ya majaribio mbalimbali ya kisayansi bali ni sifa alizonazo mwanamke.

Kwenye maumbile hatuwezi kufanana iwe kwa wanawake au wanaume, kuna wenye maumbile madogo na wengine makubwa.

Wenye makalio madogo na makubwa wote wana majina yao ya utani, wenye makalio madogo wengine huwaita flat screen wakifananishwa na wembamba wa runinga zenye kioo cha wima (flat) ama wamepigwa pasi wakiwa wanamaanisha maumbile yao wamenyooka moja kwa moja ila wale wenye maumbile makubwa ndiyo hao ambao wamepewa sifa ya kuwa chura.

Nikiri wakati mwingine na mimi huwa nakaa kwenye vijiwe mitaani hata vile vya kahawa na nikiwa hapo huwa nachangia mijadala, naibua hoja, nanogesha soga ilimradi tu mjadala wa kijiwe uende.

Na katika moja ya mijadala iliyoibuka siku kwenye kijiwe kimojawapo ni sababu ya wanaume kupenda wanawake wenye makalio makubwa.

Kukinzana kwa hoja kwenye mjadala hapo kijiweni kulinifanya nirudi kufanya uchunguzi wa kisaikolojia na kujua kwa kina kipi kinasababisha hali hiyo.

Kama ilivyo mimi nilivyopigwa na butwaa baada ya mjadala huo kuibuka ndivyo walio wengi hujiuliza kwanini baadhi ya wanaume hupenda wanawake wenye maumbile hayo.

Kwenye tovuti ya BBC Swahili, Februari mwaka 2015, waliandika habari yenye kichwa habari Utafiti: Wanaume wanapenda wanawake wenye makalio makubwa. Utafiti huo ulifanywa na vyuo vikuu vya Bilkent, Texas, na American University kilichoko mjini Beirut.

Kwenye utafiti huo ilionekana kwamba, kinachowavutia wanaume si tu makalio makubwa bali ni kupinda kwa uti wa mgongo na BBC Swahili ikaongeza kuwa kinachowavutia zaidi ni kupinda kwa uti wa mgongo unaosababisha makalio kuonekana zaidi.

Vilevile utafiti huo ulionyesha kuwa, katika miaka ya awali mwanamke aliyeonekana kuwa na maumbile hayo makubwa alipendelewa kutokana na uwezo wake wa kubeba mizigo mgongoni. Pia kwenye habari hiyo ya kitafiti ilielezwa kuwa aliwavutia wanaume wengi na hivyo kuwa na uwezo wa kuzaa watoto wengi.

Pia nukuu ya Dk. John Lehmiller ambaye ni mwanasaikolojia aliyoiandika kwenye makala yenye kichwa cha habari “The Science Behind Men’s Attraction To Women's Rear Ends” iliyochapwa kwenye tovuti yake, aliandika kuwa “kwa muda mrefu wanasaikolojia wa kimapinduzi wamekuwa na mjadala kuwa mambo mengi yanayaowavutia wanaume kwa wanawake yanahusisha sifa za muonekano wa maumbile yao na uwezo wa kuzaa.

Tabia hii ya wanaume kuvutiwa na maumbile ya wanawake hususani makalio siyo ya jana wala juzi ni ya vizazi vingi ndiyo maana Dk. Lehmiller alilithibitisha hilo kwa kusema sababu hizi za wanaume ziwalivuta wahenga na wahenga kwa hoja kuwa zinachochea hamu ya kujamiiana.

Kuna utafiti mwingine uliofanywa na wataalam wasaikolojia kutoka nchini Malaysia na kutaja sababu nyingine ambayo ni tofauti na iliyotolewa na Dk. Lehmiller. Watafiti hao wanasema wanaume wanaopenda wanawake wenye makalio na matiti makubwa ni wale wenye kipato duni zaidi ya wanaume ambao walioridhika kifedha na mali

Wanataja sababu kubwa iliyowapelekea wanaume hao kuchagua wanawake wenye maziwa na makalio makubwa ni ishara ya kisaikolojia kuwa wanawake wenye maumbile hayo ni hazina kubwa ambayo huwafanya watengeneze picha ya ukubwa wa hazina kwenye ubongo wao.

Kwenye utafiti huo ulitumia sampuli ya wanaume 266 nchini humo, wengi kutoka jamii ya watu wa kipato cha chini waliwataja wanawake wenye maumbile hayo kama wenye mvuto zaidi huku wale waliotoka kwenye maisha bora walichagua wenye maziwa na makalio madogo au ya wastani.

Pamoja na tafiti hizo kuibua mijadala na mitazamo tofauti pia kumemuibua mwanasaikolojia mwingine, Dk. David Lewis, ambaye ameongeza jambo lingine kwenye hili kwa kusema wanaume wanaofikiria makalio makubwa ya wanawake huwa wanawaza zaidi namna mgongo wa mwanamke ulivyopinda ili umbile lake lionekane vizuri.

Hulka hii ya wanaume imewaathiri pia na wanawake wenyewe kwa kudhani kuwa na makalio makubwa kunawavutia na kuwadhibiti wanaume wao huku baadhi ya akina dada hufanya kila liwezakanalo kuhakikisha wanakuwa na makalio makubwa wengine wakidiriki hata kufanya upasuaji au kutumia dawa za kisasa ili kutengeneza umbo au shepu mpya yenye makalio makubwa. Jifikirie uko wapi.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad