Kocha msaidizi wa timu ya taifa ya Tanzania, 'Taifa Stars' Hemed Morocco, amesema wamepokelewa vizuri na hakuna figisu zozote walizofanyiwa mpaka sasa kwenye kambi yao huko nchini Cape Verde.
Morocco amebainisha kuwa walipofika jana mchana wakapewa huduma na maelekezo yote ikiwemo uwanja wa kufanyia mazoezi ambao kwa mujibu wa taratibu za FIFA utakiwa kuwa uwanja ambao utachezewa mchezo husika na wao wamefanyiwa hivyo.
''Kiukweli hakuna figisu tangu tulipofika jana, tumepewa uwnja wa taifa ambao tutachezea mechi na ndio tumefanyia mazoezi ya jana jioni, kitu ambacho ni kizuri kwetu kuelekea mchezo huu wa muhimu'', amesema.
Mbali na hilo Morocco ambaye pia ni kocha mkuu wa Singida United amesema wachezaji wote wapo vizuri na wana ari ya mchezo wakionesha ushindani mkubwa kwenye mazoezi.
Kila mchezaji anajituma sana kwenye mazoezi, ushindani ni mkubwa kila mmoja anaonesha uwezo wake ili kujaribu kuona kama wanaweza kupata nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza hicho ndio kitu kikubwa tunachojivunia sisi kama walimu.
Taifa Stars na Cape Verde zitacheza mchezo wa kundi L kuwania kufuzu AFCON 2019, kesho Oktoba 12, 2018 kabla ya kurejeana Jumanne Oktoba 16, 2018.