Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini Anthony Komu amemkosoa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi Humphrey Polepole akidai kiongozi huyo ni muongo na hajawahi kuongea nae mipango ya kuhamia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Akizungumza na www.eatv.tv juu ya kauli hiyo ya Polepole, Anthony Komu amedai kuwa tangu awe mbunge amekutana na Polepole mara moja tu na hajawahi kuzungumza nae jambo lolote.
Komu amesema “Polepole ni muongo sana licha tu ya kuhusiana na jambo hili, hata masuala mengine sitaki kuongea nae hata kidogo, lakini hata kama ningeomba kujiunga na CCM na wangenikatalia ni ubaguzi wa namna yake kama ingekuwa ni kweli, mtu anapojiunga na chama hakuna vigezo kama anafanya kitu gani kwenye majimbo yao.”
“Mimi na Kubenea tulishasema hatuwezi kwenda CCM, na kama analifahamu jimbo langu vizuri asingeweza kuzungumza kitu kama hicho, kifupi tuna maendeleo sana kwenye jimbo la Moshi vijijini yeye anakaa mjini hawezi kujua maendeleo ya Moshi na mengine najiandaa kwa ajili kukabidhi kwa serikali kama mchango wananchi wa Moshi vijijini kwa serikali.” Ameongeza Mbunge Komu.
Mwishoni mwa juma lililopita akiwa moja ya mikutano ya CCM katika wilaya Temeke Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Polepole alisema “ wamewalazimisha waliokuwa wasema ukweli waombe samahani, wangekuwa wazuri wameomba kuja ila tumewakatalia sababu kwenye majimbo yao hawatoshi.”