Marwa Itembe (28), mkazi wa kijiji cha Mbalimbali wilayani Serengeti Mkoa wa Mara amefikishwa mahakamani kwa makosa matatu ya uhujumu uchumi.
Mbele ya Hakimu mkazi mfawidhi wilaya ya Serengeti Ismael Ngaile, mwendesha mashtaka wa Polisi, Paskael Nkenyenge jana Jumanne Oktoba 9, 2918 alisema mshtakiwa alikamatwa na miguu miwili ya nyumbu yenye thamani ya Sh1.4milioni.
Akisoma hati ya mashitaka katika kesi ya uhujumu uchumi namba 111/2018 alisema kosa la kwanza ni kuingia ndani ya hifadhi ya Taifa, la pili ni kupatikana na silaha za jadi panga na kutega wanyamapori ndani ya hifadhi kinyume cha sheria.
Alisema kosa la tatu ni kumiliki nyara za Serikali baada ya kukutwa na miguu miwili ya mnyamapori huyo ikiwa na thamani ya Sh1.4milioni kinyume cha sheria.
Ametenda makosa hayo Oktoba 7, 2018 katika eneo la Nyamburi ndani ya hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Mshtakiwa huyo hakutakiwa kujibu chochote na amerudishwa mahabusu hadi Oktoba 23, 2018 kesi hiyo itakapotajwa tena.