WABUNGE wawili wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Saed Kubenea (Ubungo) na Anthony Komu (Moshi Vijijini), wamewaomba radhi viongozi na wanachama wa chama hicho kufuatia ujumbe wao wa sauti kusambaa mitandaoni ukiwa na mazungumzo yaliyolenga kukichafua chama chao.
Wabunge hao wameomba radhi leo Alhamisi, Oktoba 18, 2018 mbele ya Kamati Kuu ya chama hicho wakati wa mkutano na wanahabari jijini Dar es Salaam baada ya wabunge hao kuitwa mbele ya kamati hiyo kujieleza kuhusu sauti hizo ambapo wote walikiri kuwa sauti zilizosikika ni zao.
Kamati hiyo iliamua kuwapa onyo kali, kuwavua nyadhifa zao zote ndani ya chama na hivyo kubakiwa na ubunge pekee, pia nimewaweka kwenye uangalizi wa mienendo yao ndani ya chama kwa muda wa mwaka mmoja.
“Yaliyotokea ilikuwa bahati mbaya sana na hatukuwa na nia ovu yoyote, naomba radhi sana kwa wanachama na Watanzania wote kwa kilichotokea. Mimi ni imara, waambieni CCM sifanani nao. Mimi kupita vigingi vyote hivi, kuja mbele ya Kamati Kuu ni ishara kwamba nipo Chadema, waliokimbilia CCM hawakuwahi hata kufika mbele ya kamati kuu, wengine walisimamishwa tu uongozi wakakimbia.
Baada ya wawili hao kuomba radhi, baadhi ya maswali waliyoulizwa na waandishi wa habari ni kuhusu:
Kupotea Ben Saanane na gazeti la Mwanahalisi kuandika ‘yupo vijiweni’
Kubenea alijibu: “Kuhusu Ben Saanane nimesikitika, mimi ni mmiliki wa gazeti japo ni mwandishi, MwanaHALISI ina wahariri wake na wala sikuandika mimi stori hiyo. MwanaHALISI inafuata misingi ya uandishi na ni gazeti ‘serious’. Suala hilo waulizwe wahariri, sihusiki na gazeti hilo.
Kuhusu uhusiano wake na Meya Boniface Jacob
“Mimi ni Mbunge wa Ubungo, (Boniface) Jacob ni Meya wa Ubungo, hatuna mgogoro na Jacob. Tunafanya kazi pamoja na kushirikiana bila shida yoyote. Jacob ni miongoni mwa marafiki zangu wa karibu,” alisema Kubenea.
Kauli ya Komu
“Ninakishukuru chama kwa kulipa uzito suala hili, nakubali kuwa chama ni kikubwa kuliko sisi wote. Nitayatekeleza yote yaliyoelekezwa mara moja, naomba radhi kwa chama, wanachama na Watanzania kwa ujumla. Mazungumzo yale yalikuwa ya faragha lakini teknolojia ilinizidi ujanja, nawaomba radhi Mheshimiwa Freeman Mbowe na Meya wa Ubungo, Boniface Jacob, kwa kilichotokea. Tunataka tuanze upya.”