Kuna Faida na Hasara pia Endapo Kutakua na Majibizano kwenye mahusiano


Sidhani kama kuna ambaye hajawahi kujikuta kwenye majibizano na mpenzi wake. Hata wakati mnaingia katika mlipuko wa majibizano hata mnashindwa kujua sababu ya kujibizana kwenu. 

Vitu kama vile mmoja kuchelewa kurudi nyumbani, kushindwa kuwasiliana sawa na mwingine alivyotarajia, kushindwa kutoa msaada pale ulipohitajika, hisia za kuwapo kwa mahusiano pembeni, tabia zisizoeleweka baina ya mmoja na simu yake ya mkononi au ndugu zenu kuingilia uhusiano wenu kwa namna yoyote ile. 

Haya ni baadhi tu ya maeneo ambayo wengi wetu tumejikuta tunapishana kimaneno na wapenzi wetu. Mara nyingine inatokea mmepanga kwenda kula au kunywa nje ya nyumbani “outing” mnafika tu sehemu husika mkiwa mnasubiria chakula au mmeshaanza kula mara mmoja wenu anatoa neno moja linaloamsha majibizano makali na ghafla raha ya kuendelea kuketi na kula pale inaisha, mnaamua kukiacha chakula na kuondoka tena ikiwezekana kila mmoja kwa njia yake. 

Najua kama ingekuwa tuko darasani nikasema wanyooshe mikono wale ambao hali kama hizi au zinazofanana na hizi zimewahi kuwatokea wengi wangenyoosha mikono. 

Inabidi kuwa makini kwasababu kutofautiana katika maneno kunaweza kuwa na muendelezo bila hata ya nyie kugundua na baadaye kuwapeleka pabaya. Kwa mfano, wapenzi hawa wawili wanaanza taratibu katika maongezi yao “leo tunakula nini” mmoja anauliza, mara anajibiwa “kwanza kila ukimaliza kula unaacha vyombo mezani badala ya kunisaidia hata kuvisogeza wakati unajua tuko wawili tu?” 

Baada ya muda kupita na majibizano kama haya kuendelea, mmoja anaanza kuchoka na kumwambia mwenzake “mimi naona tunatofauti kubwa sana kwenye mambo ya majukumu ya hapa ndani na kwa jinsi hii sioni kama tutawezana bora kila mtu afuate ya kwake”. 

Hapa unaona kuwa majibizano yaliwahi kuanza muda mrefu huko nyuma ila yalikuwa na muendelezo hata pasipo wapenzi hawa kugundua na hivyo kuwasababisha kutengana. Kutofautiana katika maneno na mpenzi wako kunauma na unaweza ukatamani kufungua mlango wa gari likiwa katika mwendo utoke ili tu uondokane na kinywa chake. 

Hali hii inapozidi unaweza kujikuta unatilia shaka uhusiano wenu na kuanza kuwa na hisia za uhusitisha. Lakini hatuwezi kuukwepa ukweli kwamba majibizano na kutofautiana ni kitu cha asili kwenye uhusiano wowote. 

Jambo hili limetiliwa mkazo na wataalamu wengi wa uhusiano akiwamo mshauri Beth Fitzpatrick. Tafiti zinaonyesha kwamba wapenzi wengi wanaohudhuria huduma za ushauri wamekiri kwamba matatizo kama vile mawasiliano mabovu, kushindwa kusikiliza, kutojali, kupinga kila kinachosemwa au kutendwa na kutumia lugha za matusi yamekuwa yakudumu katika uhusiano wao. Yamkini hali hii ipo pia katika uhusiano wako. 

Kama nilivyokwisha kusema awali, kule kupitia katika majibizano hakumaanishi kwamba uhusiano wenu unamatatizo, kinyume chake ni kwamba uhusiano wowote usipopitia majibizano na kutofautiana unaweza kukosa ubora unaotakiwa kiuhusiano au kindoa. 

Mara nyingine wapenzi wanaosema hawajawahi kutofautiana au kugombana wana madhaifu mengi tofauti na wanavyoonekana. 

Kukosa mazingira ya kutofautiana katika uhusiano kunaweza kuwa na madhara makubwa kuliko kuwa na mazingira ya kutofautiana, wenye kukosa kutofautiana kimaneno wanaweza kuwa na tabia kama ukatili wa kimyakimya, kununiana na kunyimana tendo la ndoa. 

Tabia hizi zina madhara katika uhusiano. Kama mazingira ya kutofautiana yapo na ni dhahiri, kwa nini msitofautiane? Cha muhimu ni kuchagua kutofautiana kwa namna inayojenga na sio inayobomoa.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad