Majambazi Yaliyoiba Gari Jijini Dar Yanaswa Jijini Mwanza


Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza tumewakamata Majambazi wawili kwa kosa la wizi wa gari lenye namba T.929 DCD aina ya HINO mali ya kampuni ya Sonu East Africa ltd ya Jijini Dar es Salam huko Kishiri –Igoma Wilaya ya Nyamagana Jiji na Mkoa wa Mwanza, kitendo ambacho ni kosa kisheria.

Ukamataji huu, umefanyika tarehe 11/10/2018 majira ya saa 17:00hrs jioni, hii ni baada ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza kupata taarifa za kiintelejensia kwamba katika Mkoa wa Mwanza wameingia majambazi wakiwa na gari la wizi ambalo wameliiba toka Jijini Dar es Salam.

Baada ya kupatikana kwa taarifa hizo Polisi tulianza ufuatiliaji wa  chocho kwa chocho na maeneo mbalimbali ya Jiji la Mwanza na kufanikiwa kukamata wezi hao wakiwa na gari hilo tajwa hapo juu huko maeneo ya Kishiri –Igoma hapa Jijini Mwanza.

Gari hilo liliibiwa tarehe 24/09/2018 huko maeneo ya Kimara Jijini Dar es Salaam, ambapo baada ya kuibiwa tarehe 25/09/2018 taarifa zilifika kituo cha Polisi Kimara na kufunguliwa kesi kisha ufuatiliaji ulianza kufanyika lakini baadae ilibainika kuwa wezi hao wamekimbilia Jijini Mwanza wakiwa na gari hilo.

Watuhumiwa waliokamatwa ni 1. Saraji Ezekiel, miaka 44, Mkazi wa Kimara – Dar es Salaam, dereva wa gari  ambaye ndiye alieliiba gari hilo toka Jijini Dar es Salaam na kuja nalo Mwanza na 2. Karimu Hussein, miaka 30, Mkazi wa Kishiri – Igoma, ambaye ndiye aliyekuwa kondakta wa gari hilo. Wezi hawa baada ya kufika hapa Jijini Mwanza wakiwa na gari hilo walifuta majina ya ruti ya gari hiyo ambayo ilikuwa imeandikwa Mbezi – Makumbusho

Pia gari hilo walilipeleka kwenye garage mbili hapa Mwanza kwa ajili ya kulikata vipandevipande ili baadae waliuze, lakini wamiliki wa garage walikataa na kuwaeleza kuwa wanamuogopa Afande RPC wa Mwanza. Vilevile walikuwa wakibeba abiria nyakati za usiku kwa ajili ya kujipatia fedha.

Polisi tunaendelea na upelelezi pamoja na mahojiano na watuhumiwa wote wawili pindi uchunguzi ukikamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza, tunatoa onyo kwa wezi na wahalifu wote kwamba wakiingia Mwanza hawatatoka hivyo waache kwani tutawakamata na kuwashughulikia kwa mujibu wa sheria. 

Pia tunaendelea kuwasisitiza wananchi waendelee kutupa ushirikiano kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu ili waweze kukamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad