Makala: “Alikiba Unakua Kiumri Kimuziki Unadumaa Badilika Utapotea”



Wahenga walisema muda ni ukuta hauwezi kushindana nao, na hii inakuja kujionesha hata katika maisha ya kawaida kadri muda unavyozidi kwenda vitu kama mitindo, teknolojia na hata ladha ya muziki nayo inabadilika, lakini sio kwa msanii wa muziki wa Bongo Fleva, King Kiba.

Alikiba bado anaamini kuwa nyimbo zake za zamani alizowahi kuziachia iwe kwa kuvujisha au kuziachia mtandaoni, kwa muda huo zinaweza kutumika tena na ku-hit jambo ambalo sio baya kwa msanii lakini kwa mtu mkubwa kama Alikiba huo ni uvivu.

Hebu turudi nyuma kidogo, Alikiba kwa miaka mingi alikuwa kimya kwenye muziki lakini mwaka 2014 aliporudi kwenye gemu na kuanza kutoa nyimbo kama Mwana (2014), Chekecha Cheketua (2015), Aje (2016), Seduce Me (2017) na Nagharamia watu wengi walianza kumuelewa na aliongeza mashabiki wapya ambao kwa miaka 2006 wakati anafanya vizuri wengi walikuwa ni wadogo kiumri.

Kutokana na ukubwa wa nyimbo hizo alizoachia kwa miaka mitatu mashabiki wengi wapya walianza kumfuatilia na kuamini kuwa wapo upande sahihi, lakini sio kwa mwaka 2018.

Kwa mwaka huu 2018 Alikiba umewakosea mashabiki wako wapya na hata baadhi ya mashabiki wako wa zamani, kwani nyimbo zote tatu hakuwa wimbo uliopokelewa vizuri kama zile ulizoachia miaka mitatu ya nyuma.

Wimbo kama Mvumo wa Radi sidhani kama unaweza ukaufananisha na Mwana, au wimbo kama Maumivu Per Day unaweza ukaufananisha na Aje au pengine wimbo wake mpya wa Hela unaweza ukaufananisha na Seduce Me.

Hii ni ishara tosha Alikiba kwa mwaka huu umewaangusha mashabiki wako, ngoma zote ulizotoa zimepokelewa kawaida sana.

Na, pengine huenda asiwe yeye peke yake aliyetoa nyimbo za kawaida kwa mwaka huu lakini, tunakuzungumzia yeye kutokana na ukubwa wa jina lake ‘KING KIBA’.

Achilia mbali, mashabiki wengi wa Alikiba ni wakubwa kimri kuanzia miaka 25 na kuendelea, lakini hiyo isimfanye Alikiba kubweteka na kutoa nyimbo za kawaida kama Mvumo wa Radi, Hela na Maumivu per Day.

Nyimbo kama Hela na Maumivu Per Day zote Alikiba alishawahi kuziachia mtandaoni miaka ya nyuma na zimesikilizwa hadi watu wakazichoka, sasa ni uvivu gani hadi akaamua kuziachia tena ile hali anajua muziki wa sasa unahitaji ubunifu wa hali ya juu ili usikilizwe zaidi.

Alikiba ni msanii mwenye kila sifa ya kuitwa msanii mkubwa, anauwezo wa kuandika nyimbo na kabarikiwa sauti, sasa ni kitu gani kinachomfanya mpaka arudie nyimbo kama Maumivu Per Day na Hii aliyoichia leo ya Hela? bila shaka ni uvivu.

Kwa jinsi muziki wa sasa ulivyo kiushindani, Alikiba usitegemee mashabiki wako wapya watashindwa kukushambulia endapo utaendelea kutowatendea haki kwa kuachia nyimbo za kawaida au kurudia nyimbo za zamani.

Leo, Alikiba ameachia wimbo wake aliyouita mpya wa ‘HELA’ ambao kiukweli sio mpya ni wimbo wa miaka mitatu iliyopita na hata kipindi hicho haukuwa mkali kivile, sasa kwanini unakuja kuurudia mwaka 2018?

Sitaki kuamini kama Alikiba ni mvivu kiasi hicho au ameridhika kiasi kwamba anashindwa kuumiza kichwa na kutunga nyimbo kali kama alivyozoeleka.

SOURCE: Bongo 5

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad