MAMA mzazi wa aliyekuwa mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya Deutsche Welle (DW) nchini Ujerumani, marehemu Isaac Muyenjwa Gamba, amepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha mwanaye huyo.
Mama huyo alikuwa akizungumza na Global Digital baada ya mwili wa mwanaye kuwasili nyumbani, Bunda mkoani Mara kwa ajili ya amzishi ukitokea Dar es Salaam kupitia Mwanza, jana Jumanne, Oktoba 30, 2018.
“Alipokuja mara ya mwisho alisema hatokaa siku nyingi, aliniambia ‘Mama nitakaa siku tatu tu kwa sababu nina ujenzi wa nyumba yangu Dar es Salaam, nitamaliza majuma mawili nikiwa kule’ siku anaondoka aliniaga, akaenda Ujerumani’,” alisema mama huyo na kuongeza:
“Mwanangu Isaac alikuwa mcheshi na mpenda watu, hakuwa mgomvi tangu akiwa mdogo, wakati alipokuwa akija huku nyumbani alikuwa hachagui wa kumpa zawadi, mimi mama yake, dada zake na watoto wa dada zake wote alikuwa anawagawia zawadi bila ubaguzi, kifo chake kimeiacha familia katika isiyoelezeka kutokana na upendo wake kwa familia na ndugu zake.
“Mwanangu alipenda sana mpira tangu akiwa shule, kuna mtangazaji mmoja nimemsahau jina, alikuwa anampenda sana, akawa anasema ‘Mama nikimaliza shule ninataka nije kuwa mtangazaji’, kweli alipomaliza huku alikwenda Arusha kwa kaka yake ndiko alianzia utangazaji, baadaye alikuja Mwanza, kisha Dar es Salaam na hatimaye akaenda Ujerumani.”
Gamba alikutwa amefariki chumbani kwake Alhamisi, Oktoba 18, mwaka huu, jijini Bonn nchini Ujerumani alikokuwa akifanya kazi zake. Baada ya uchunguzi wa hospitali nchini Ujerumani, imegundulika kuwa kilichosababisha kifo chake ni kuvuja kwa damu kwenye ubongo (Brain Hemorrhage) yaani presha ya damu, atazikwa leo nyumbani kwao Bunda, Mara.
Mama Mzazi wa Issac Gamba Afunguka Alichoongea Mara ya Mwisho na Mwanaye Kabla ya Kifo
0
October 31, 2018
Tags