Manispaa K’ndoni yapewa siku 57 kukamilisha Barabara Tegeta Nyuki


Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, imetakiwa kukamilisha ujenzi wa kipande cha Barabara ya Tegeta Nyuki kuelekea Kunduchi yenye urefu wa kilomita 2.2 ndani ya siku 57. 

Ujenzi wa barabara hiyo umefikia asilimia tatu tu wakati ulitakiwa uwe umefikia asilimia 80 na kukabidhiwa kabla ya Novemba 29, mwaka huu. 

Agizo hilo lilitolewa jana na Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Joseph Kandege, baada ya kufanya ziara katika barabara hiyo na kutoridhishwa na kasi ya ujenzi. 

“Nilitarajia leo nikute barabara imekamilika, lakini hadi sasa bado na naambiwa inatakiwa ikamilike Novemba 29, mwaka huu, sasa sijui mtafanyaje ila nataka ikabidhiwe tarahe iliyopangwa, mi sijui mtafanyaje ila ikamilike na nitakuja mwenyewe hapa nikute barabara imekamilika," alisema Kandege. 

Alisema barabara hiyo inatakiwa kukamilika kwa wakati ili kupunguza adha wanayopata watumiaji hasa wakati wa mvua. 

Aidha, Kandege alitembelea barabara ya Mikocheni eneo la ITV na kusema kuwa ameridhishwa na utendaji kazi wa mkandarasi na kuahidi kuwa itaendelea kuboreshwa kwa kuiwekea zege. 

Pia alitembelea soko la Magomeni usalama na kuagiza ujenzi wake uanze haraka iwezekanavyo ili kuweka mazingira mazuri ya wafanyabiashara kufanya shughuli zao. 

Kandege pia alitembelea Kituo cha Afya cha Kigogo na kukagua jengo la wodi ya wazazi iliyoungana na chumba cha upasuaji kwa wajawazito linalokarabatiwa na serikali kwa Sh. milioni 400 zinazotolewa kwa ajili ya kujenga vituo vya afya kila wilaya nchini. 

Katika jengo hilo ambalo awali lilikuwa likitumiwa na kituo cha kulelea watoto yatima cha Dogodogo Centre, Naibu Waziri huyo aliagiza kazi hiyo ikamilike haraka. 

Pia aliagiza uongozi wa wilaya hiyo ufanye mazungumzo na majirani wanaoishi eneo hilo, ili wanunue tena eneo lingine kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa majengo ya kituo hicho cha afya. 

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Daniel Chongolo, alisema atayafanyia kazi maagizo yote aliyopewa na Naibu Waziri na kuahidi kuwa Jumatano  wiki ijayo atarudi kukagua mradi wa ujenzi wa soko la Magomeni. 

“Ushauri au mapendekezo yaliyotolewa na Naibu Waziri ni maagizo ambayo natakiwa kuyafanyia kazi haraka sana, nitahakikisha nasimamia utekelezaji wake," alisema Chongolo. 

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad