Hivi sasa mashabiki na wadau wa soka Tanzania wamejawa na matumaini juu ya timu yao ‘Taifa Stars’ katika safari ya kufuzu michuano ya mataifa ya Afrika AFCON mwakani nchini Cameroon, baada ya kuichapa Cape Verde hapo jana.
Stars ilishinda kwa mabao 2-0 na kuweka hai matumaini ya kufuzu michuano hiyo, mabao yaliyofungwa na nyota wake Simon Msuva na Mbwana Samatta. Samatta alionesha kiwango kikubwa na kizuri katika mchezo huo hasa baada ya kukosa mkwaju wa penalti, ambao ulimpa nguvu na ari ya kupambana ili kuiokoa timu yake.
Juhudi yake iliipa mafanikio Stars ambapo baada ya mchezo huo kila mmoja alionekana kumpongeza na kusahau machungu ya bao alilolikosa. Hapa tumekusogezea mambo manne ambayo aliyafanya Samatta mara baada ya kumalizika kwa mchezo huo.
Kufutwa kiatu na moja ya kiongozi, Samatta aliwakosha wengi waliokuwa uwanjani katika mchezo huo ambapo katika tukio lisilotarajiwa, kiongozi mmoja wa benchi la ufundi la Taifa Stars alionekana akimfuta kiatu chake na mguu wake kuonesha ishara ya kukubali alichokifanya uwanjani huku Samatta mwenyewe akifurahi.
Kwenda kushangilia na mashabiki, mashabiki wa soka wa Tanzania wanapenda sana timu yao ya taifa hasa inapofanya vizuri, hilo limejidhihirisha jana ambapo baada ya mchezo huo mashabiki walimtaka samatta kwenda kuwapungia mkono na kumpongeza kwa shughuli aliyoifanya, jambo ambalo ni mara chache sana limetokea katika mechi za hivi karibuni za Taifa Stars.
Alipolizungumzia bao alilokosa, baada ya kumalizika kwa mchezo huo, Samatta akiwa mwenye furaha alisema kuwa kukosa kwa mkwaju wa penalti kulimfadhaisha kwa muda mfupi lakini alijua anatakiwa kufanya kitu kikubwa zaidi ya nafasi ambayo aliikosa kwasababu muda bado ulikuwepo.
Kuwashukuru mashabiki akiwa uwanja wa ndege, Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Samatta ameandika ujumbe majira ya saa 9 za usiku akiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere akiondoka kuelekea Ubelgiji, amesema “Goli, assist na ile ingine wacha ibaki siri yetu. Niko proud sana na wachezaji wenzangu ,makocha pamoja na mashabiki wote katika mchezo wa leo kwa umoja na mshikamano. ”