Wanasayansi nchini Uingereza na Gambia wanasema wana ushahidi wa awali unaoonesha kuwa mbwa wanaweza kunusa malaria.
Kuna matumaini makubwa kuwa wanyama hao watatumika katika mapambano dhidi ya malaria na hatimaye kuutokomeza kabisa ugonjwa huo.
Wanasayansi Kenya wavumbua dawa ya Malaria kwa waja wazito
Kutana na wataalamu wanaozunguka Zanzibar kupambana na Malaria
Japokuwa utafiti huo upo katika hatua za awali, wanasayansi wanaamini matokeo yake yanaweza kubadili namna ya kufanya vipimo vya malaria.
Kwa mujibu wa tafiti za hapo awali, mtu ambaye ana vimelea vya malaria mwilini anakua na harufu ya tofauti ambayo inawavutia mbu kuendelea kumshambulia. Na sasa, mbwa wapo kazini kuinusa harufu hiyo.
Soksi zilizovaliwa na watoto usiku kucha katika jimbo moja nchini Gambia zilisafirishwa mpaka Uingereza kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi.
Kati ya jozi 175 zilizotumwa katika wakfu wa mbwa wa ugunduzi wa kimatibabu mjini Milton Keynes, 30 zilikuwa zimevaliwa na watoto wenye vimelea vya malaria.
Mbwa hao wenye uwezo mkubwa wa kunusa hivi sasa pia wapo kwenye mafunzo ya kunusa harufu ya saratani na ugonjwa hatari wa kukakamaa (Parkinson's disease).
Matokeo ya jumla, ambayo yalitolewa katika mkutano wa mwaka wa Jumuiya ya Amerika ya Magonjwa ya Kitropiki na Usafi yanaonesha kuwa kati ya watoto 10 walioathirika, mbwa wanauwezo wa kutambua watoto 7.
Lakini pia walifanya makosa kwa kudhani kuwa mtoto mmoja ana maambukizi kati ya 10 ambao wapo salama.
Mtafiti Mkuu Profesa Steve Lindsay, kutoka chuo kikuu cha Durham, amesema wanafuraha kubwa juu ya matokeo hayo, lakini mbwa hao bado hawajawa tayari kutumika kila siku.
Watafiti bado wanahitaji muda zaidi kuboresha umakini wa mbwa na kuanza kunusa watu badala ya soksi. Pia wanata kujiridhisha kama mbwa wanaweza kutambua aina tofauti za malaria.
Lengo ni kutumia mbwa hao siku moja katika viwanja vikubwa vya ndege ili kuzuia maambukizi. Utumiaji wa wanyama hao pia utakuwa ni hatua kubwa ktaika kutokomeza ugonjwa huo sababu haitasubiriwa mpaka mtu aoneshe dalili ndi afanyiwe vipimo kama ilivu kwa sasa.
Mbwa pia wana uwezo wa kupima kundi kubwa la watu kwa muda mchache.