IMERIPOTIWA kuwa Klabu ya Everton ambayo inashiriki Ligi Kuu ya England, ina mpango wa kumsajili mshambuliaji Mtanzania, Mbwana Ali Samatta, ambaye anakipiga katika Klabu ya KRC Genk ya nchini Ubelgiji.
Timu hiyo inataka kumsajili mchezaji huyo ili aweze kuziba pengo la Oumar Niasse ambaye anataka kutimkia ndani ya kikosi hicho.
Samatta ambaye anaonekana msimu huu kuwa moto kutokana na kufanya vyema kwenye michuano tofauti, mpaka sasa katika michuano ya Europa amefunga mabao sita huku akifunga mabao saba kwenye ligi.
Nyota huyo amekuwa kwenye kiwango bora kwa sasa na tayari msimu huu ana ‘hat trick’ mbili alisajiliwa Genk akitokea Klabu ya TP Mazembe ya nchini DR Congo.
Everton kwa sasa inasaka mshambuliaji mbadala wa Oumar Niasse, na tayari kocha wa timu hiyo, Marco Silva, ameonekana kuvutiwa na kasi wa Samatta.
Hata hivyo, jana iliripotiwa na vyombo mbalimbali vya Ulaya kuwa mbali na Everton pia West Ham United, Burnley na Brighton wamekuwa wakiwania saini ya nyota huyo kutokana na uwezo ambao amekuwa akionyesha kwa sasa.
Stori na Martha Mboma, Championi Jumatano