NA MARKUS MPANGALA
ACHANA na matokeo mazuri tuliyopata kwenye mchezo kati ya timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars dhidi ya Cape Verde Jumanne wiki hii. Achana na furaha tuliyonayo Watanzania kufufua matumaini ya kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon 2019) tukiwa tumejikusanyia pointi tano.
Hii ina maana Tanzania ina michezo miwili muhimu dhidi ya Lesotho (ugenini) na Uganda (nyumbani). Kwa vyovyote vile mechi zote mbili tunatakiwa kupata pointi 6 ili tufikishe pointi 11. Mechi ngumu itakuwa dhidi ya Uganda, lakini kupambana na Lesotho nina uhakika vijana wa Taifa Stars wanaweza kuibuka na ushindi ikiwa watacheza kwa nguvu, maarifa na kila mbinu zinazohitajika.
Mechi dhidi ya Uganda ni ngumu na inahitaji umakini na maarifa yote, kwahiyo ni lazima tushinde na lazima tusifungwe jogoo awike au asiwike.
Pambano la marudiano kati ya Taifa Stars dhidi ya Cape Verde limenionyesha kitu ambacho sikuwa makini nacho. Kitu ambacho kimenikumbusha enzi za umahiri wa klabu za Malindi, Mlandege, Kikwajuni na KMKM huko Zanzibar. Lakini kisoka, Zanzibar si ile kama ya akina Ali Nassoro, Ali Bushiri na mastaa wengineo.
Macho yangu yamemwona Feisal Salum au maarufu kwa jina la Fei Toto. Kwa umri wake bado ni kinda, ana miaka 20. Kijana huyu ana vitu adimu miguuni. Katika mchezo dhidi ya Cape Verde, aliingia kipindi cha pili na kuongeza kitu ambacho kingeiwezesha Taifa Stars kupata mabao hata manne.
Awali sikumzingatia sana. Hata mechi za Ligi Kuu sikumfuatilia sana lakini dhidi ya Cape Verde nimemtazama kwa dakika alizoingia. Nikajiuliza kwanini kocha amemhamishia upande wa kulia kiungo Himid Mao. Hata hivyo, kazi ya Fei Toto ilisisimua. Nilitamani kila wakati apewe mpira na kusogea zaidi langoni mwa adui. Ni bonge la kipaji.
Anapiga pasi za taratibu na haraka kulingana na walivyojipanga. Ni kiungo wa timu zaidi na anaanzisha shambulizi kwa mkakati thabiti. Kwa muda mfupi tu pasi zake zilikuwa za uhakika.
Alipoingia aliituliza zaidi Taifa Stars. Akaifanya izidishe kuweka mpira chini. Fei Toto hana mabavu kwa maana hatumii nguvu nyingi, ila kiufundi ni mzuri sana. Anateleza kama mlenda. Yaani pasi zake, mtazamo wake, vile anavyoipeleka timu mbele, ni utamu mtupu. Akipokea pasi au kutoa hana papara. Haonekani kuwa mwoga, yaani anawapa tabu adui kutafuta mpira.
Jinsi anavyopiga pasi zake ni ufundi mkubwa. Anapenda kuingia kwenye nafasi, hachezi ‘man to man’, akipokea na kutoa pasi huwa anampisha adui na nguvu zake, kisha anachochora kwenda mbele.
Kuna wakati wachezaji wa viungo wa Cape Verde walikuwa wanampa mkono na kucheka naye. Fei Toto naye alikuwa anapokea mkono na kucheka nao. Naamini ni vile alivyokuwa anageuka geuka kama chapati na kupiga pasi za ‘one on one’ pamoja na alivyokuwa anabadili mwelekeo. Alitumia eneo la katikati kusogeza mpira kwenda langoni mwa adui na kuongeza chachu ya mashambulizi ya pembeni.
Safu ya kiungo ya Taifa Stars ilitulia sana, hakukuwa na rafu kama awali bali ufundi wake ukawafanya Cape Verde wawe wanazunguka zunguka. Hilo liliwalazimisha viungo wa Cape Verde kurudi nyuma. Na zaidi mhimili wa Cape Verde ni nahodha wao ambaye amekuwa injini inayoendesha timu, lakini Fei Toto alimlazimisha kiungo huyo kurudi nyuma zaidi.
Kwa mtazamo wangu natamani Watanzania tumfukuze Fei Toto hapa nchini. Tuanze kelele sasa. Tuwalazimishe Yanga wamfukuze Fei Toto aende kucheza soka la kulipwa nje ya nchi.
Tuwahimize Yanga wafanye hivyo kwa maslahi yao wenyewe kwakuwa watakuwa wanauza kipaji kibichi ambacho kitawapa nafasi ya kuzikaribisha klabu nyingine kuona Yanga kama kisima cha kuibua vipaji, hivyo kutembelewa na mawakala au wawakilishi wa timu mbalimbali.
Fei Toto si wa kubaki hapa tena. Hata akianzia ligi ndogo za Ulaya sio mbaya. Lakini pia hata hapa barani Afrika akienda timu kama vile TP Mazembe, Orlando Pirate, Kaizer Chiefs, Zesco, Zamalek, Club African, Esperance si mbaya atakuwa mbali.
Kocha msaidizi wa timu ya Taifa ya Wanawake, Twiga Stars, Edna Lema, amemfuatilia Fei Toto ndani ya kikosi cha Yanga na Taifa Stars. Nilipomuulizia mtazamo wake kuhusu Fei Toto, aliniambia: “Bado ni kijana mdogo, ana muda mrefu wa kucheza mpira hapa Bongo au nje, la muhimu atengenezwe zaidi akianzia hapo hapo Yanga kwanza. Kwenda nje inawezakana na kwa umri huu safari yake ya kuwa bora itatengenezwa na atafikia mafanikio mazuri akizingatia.”
Ni wakati wa kumfukuza Fei Toto aende nje hata Afrika Kusini. Nasema hivi kwa sababu kikosi chetu angalau kinaleta hamasa pale tunapokuwa na wachezaji wanaocheza nje. Tunao Abdi Banda, Simon Msuva, Mbwana Samatta, Hassan Kessy, Thomas Ulimwengu, Rashid Mandawa, Farid Mussa na Shaban Idd Chilunda, kwa kuwataja wachache. Tunahitaji mastaa wengi nje ya nchi yetu.
AMUNIKE AMETUBU
Jambo la mwisho ni kwamba, Kocha wa Taifa Stars, Emmanuel Amunike, amesahihisha makosa yake ya mchezo wa kwanza. Uamuzi wa kumpanga Shomari Kapombe mbele ya Hassan Kessy ulikuwa sahihi na wenye tija kiufundi. Kumpanga Erasto Nyoni na Kelvin Yondani ni uamuzi ambao umekisaidia kikosi chetu. Wachezaji hao wameongeza tija na kuibua changamoto kwa wale walioachwa benchi. Pili, kocha amegundua uamuzi wa kupanga washambuliaji watatu katika mechi moja haikuwa sahihi. Mambo mengi yamebadilika katika mchezo huu. Beki mbili, beki tano, kiungo pia. John Bocco ni sehemu ya mabadiliko hayo.
VIVA TAIFA STARS