BEKI kisiki wa Yanga na Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Kelvin Yondani ameibuka na kusema kuwa, muda si mrefu atastaafu kuitumikia Taifa Stars.
Yondani amesema atastaafu kuitumikia Taifa Stars ili kupisha vijana waitumikie timu hiyo kwani kwa upande wake anaona kuna vijana wengi wanakuja vizuri.
Akizungumza na Championi Jumatano, Yondani alisema kustaafu kwake timu ya taifa ni kutoa fursa kwa wengine kwani yeye ameitumikia kwa muda mrefu na sasa ni wakati kwa wengine kuitumikia timu hiyo.
“Nimekaa na kufikiria kwamba muda wangu wa kustaafu kucheza timu ya taifa umefika na kuwapisha vijana nao waweze kulitumikia taifa lao. “Nimecheza kwa muda mrefu na nadhani watu wameona nimeifanyia nini timu yangu ya taifa, hivyo niseme tu siku si nyingi nitatangaza rasmi kustaafu.
“Nimeona kuna vijana wengi wanaocheza kwenye nafasi yangu wanakuja vizuri, hivyo ni bora kuwapisha ili waendeleze pale ambapo mimi nimeachia, naamini kuwa bado wanaweza kufanya mambo
makubwa zaidi kwenye nchi hii,” alisema Yondani.
Beki huyu ndiye mchezaji mkongwe zaidi kwenye timu ya Taifa, Taifa Stars kwa sasa akiwa ndiye ameichezea timu hiyo michezo mingi zaidi. Yondani ambaye amewahi kuichezea timu Simba alikuwa uwanjani jana wakati Stars ilipokuwa ikivaana na Cape Verde kwenye mchezo wa kutafuta tiketi ya kucheza Kombe la Mataifa Afrika.
Ukiacha kuwa na makombe mengine mengi kwenye ngazi ya klabu, beki huyo mafanikio yake makubwa kwenye timu ya taifa ni kuifikisha timu hiyo kwenye fainali za Kombe la Mataifa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (Chan), ingawa ilitolewa kwenye hatua za mwanzoni kabisa.