Mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi amekumbana na miujiza kwenye historia yake ya soka baada ya kuweka rekodi ya pekee ya kucheza dakika 360 sawa na mechi nne bila kufunga bao lolote licha ya kwamba tayari mkewe na watoto amewahamishia Dar es Salaam.
Simba mpaka sasa imecheza mechi sita na kuweza kufunga jumla ya mabao nane. Msimu uliopita timu ikiwa imecheza mechi hizo sita Okwi tayari alikuwa amefunga mabao saba ndani yake kukiwa na ‘hat trick’.
Msimu uliopita mshambuliaji huyo alifanikiwa kufunga jumla ya mabao 20 kwenye ligi na kumaliza akiwa kinara.
Okwi mpaka sasa amecheza mechi nne ambazo ni dhidi ya Yanga, Mbao FC, Mbeya City na Ndanda FC huku wakipoteza mchezo mmoja na hajatupia.
Mechi ambazo Okwi amekosa ni pamoja na mechi ile ya Mwadui FC na Tanzania Prisons.
MBELGIJI AMTETEA
Kocha wa Simba, Patrick Aussems amepooza mambo kwa kusema hali hiyo siyo ya kwanza kumtokea fowadi wake huyo kwani inawakumba washambuliaji wengi duniani.
“Ieleweke kwamba siyo yeye tu hata mshambuliaji wetu mwingine Meddie Kagere naye kwa sasa hajafunga hivi karibuni lakini hakuna shida yoyote ile ambayo unaweza kusema wanayo wao, jambo la msingi kila mmoja kwenye timu anahitajika afunge anapopata nafasi.
“Hali hiyo inatokea kwa kila mshambuliaji duniani ya kutokufunga kwenye mechi moja au kukosa nafasi nyingi kwenye mechi.
Lakini siyo hilo tu pia inatokeaga kwa mshambuliaji kushindwa kufunga hata mechi mbili au tatu mfululizo hilo jambo la kawaida sana, watu waelewe tu kwamba wakishindwa wao kufunga wengine nao wanatakiwa kuchukua jukumu hilo ili waweze kufunga,” alisema Mbelgiji huyo.