Mfanyabiashara, Akram Azizi Abdul Rasool amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na makosa 75, ikiwemo kukutwa na Nyara za Serikali na utakatishaji fedha wa U.S.D 9018.
Mfanyabiashara huyo ambaye ni mdogo wa Rostam Azizi anakabiliwa na kesi ya uhujumu namba 82/2018 ambapo katika makosa yake, mawili ni kukutwa na Nyara za serikali, kukutwa silaha makosa 70, kukutwa na risasi makosa mawili ambazo ni zaidi ya (6496) na utakatishaji fedha 1.
Mshtakiwa huyo amesomewa mashtaka yake na Wakili serikali Mkuu, Paul Kadushi akisaidiana na Faraja Nchimbi mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustino Rwizire.
Miongoni mwa mashtaka aliyosomewa ni kukutwa na nyara za serikali, ambapo anadaiwa amelitenda October 30, 2018 maeneo ya Oysterbay Dar es Salaam ambapo alikutwa na Meno 6 ya Tembo yakiwa na thamani ya Shilingi MIL. 103.
Pia anakabiliwa na kosa la kukutwa na nyama ya Nyati, Kilogramu 65 yenye thamani ya Shilingi Mil 4.35 bila kuwa na kibali, ambalo amelitenda October 30,2018 sawa Oysterbay Kinondoni Dar es Salaam.
Pia anakabiliwa na kosa la kukutwa na risasi 2404, kosa ambalo amelitenda October 30,2018 maeneo ya Oysterbar DSM.
Kosa jingine ni kukutwa na silaha aina ya Pistol, ambalo amelitenda October 30,2018 maeneo ya Oysterbay Dar es Salaam bila kuwa na kibali cha Mrajisi wa Silaha.
Kosa jingine ni utakatishaji fedha wa Dola za Kimarekani 9,018 ambalo amelitenda October 30,2018 huku akijua fedha hizo ni zao la kujihusisha na makosa tangulizi.
Baada ya kusomewa makosa hayo, mshtakiwa hakuruhusiwa kujibu kitu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka.
Upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika, mshtakiwa amerudishwa rumande, kesi imeahirishwa hadi November 12,2018.