Mhadhiri UDOM anaswa na Takukuru kisa rushwa ya ngono


Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa mkoa wa Dodoma TAKUKURU, inamshikilia mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) Jacob Nyangusi, kwa kosa la kumtaka kingono mwanafunzi wa mwaka wa kwanza ili amsaidie katika mitihani. 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Dodoma Sostenes Kibwengo, Mhadhiri huyo wa Kitivo cha Sayansi ya Jamii katika Chuo Kikuu cha Dodoma ametenda kosa hilo kinyume na kifungu cha 25 cha Sheria ya kuzuia na Kupambana na rushwa Na. 11/2007. 

Kibwengo amesema kuwa Mhadhiri huyo alikamatwa saa tatu usiku katika eneo la nyumba mia tatu kata ya Nzuguni jijini Dodoma akiwa chumbani na mwanafunzi huyo. 

Amesema Takukuru ilipokea taarifa za Mhadhiri huyo kutaka rushwa ya ngono kwa mwanafunzi wake (jina limehifadhiwa), ili amwezeshe kufanya mitihani ya marudio baada ya kufeli na pia amsaidie wakati wa usahihishaji. 

Amesema baada ya kupokea taarifa hizo Takukuru ilifanya uchunguzi wa awali na kuandaa mtego uliofanikisha kukamatwa kwake. 

Takukuru inaendelea na uchunguzi na mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani pindi kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kikitolewa.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad