Msanii wa muziki wa HipHop nchini, Nickson Simon maarufu kama 'Nikki wa Pili' ameelezea masimamo wake katika siasa kufuatia maoni mbalimbali ya mashabiki wanaomtaka kujiunga rasmi na chama cha siasa baada ya hivi karibuni kutangaza nia yake ya kutaka kugombea Urais.
Akipiga stori na www.eatv.tv, Nikki amesema kuwa hatosikiliza watu wanasema nini katika mipango yake ya maisha na kusisitiza kuwa kwa sasa hayupo katika chama chochote zaidi ya chama cha wananchi ambao ni wengi nchini.
“Nafikiri maisha hutakiwi kuishi vile ambavyo watu wanataka,inabidi kuishi vile ambavyo wewe unataka ukiangalia kila siku watu wanasema nini huwezi endelea na mimi nilisha sema sipo chama chochote, mimi nashabikia chama cha wananchi”, amesema Nikki wa Pili.
Pia msanii huyo amesifu juhudi zinazofanywa na Rais Magufuli katika utekelezaji wa miradi mbalimbali nchini ikiwemo miundombinu ya barabara na miradi mikubwa ya umeme.
“Kwa upande wa rais Magufuli mi naona ni Rais mwenye msimamo,na mambo mengi ambayo anataka anatekeleza, hususani katika miradi mbalimbali ya kimaendeleo kama flyover, ambayo wote tumeiona, uwanja wa ndege punde unakaribua kuisha, mradi wa umeme wa Kinyerezi pamoja na 'Stiegler's Gorge' mradi wa kuzalishia umeme”, ameongeza.