Mke wa Rais wa Marekani Melania Trump Apokelewa Mapokezi ya Aina Yake Kenya

Mke wa Rais wa Marekani Melania Trump Apokelewa Mapokezi ya Aina Yake Kenya
Mke wa Rais wa Marekani Donald Trump, Melania, aliwasili Kenya Alhamisi jioni kwa awamu ya tatu ya ziara yake ya kwanza rasmi Afrika. Alilakiwa uwanja wa ndege na Mama wa taifa Margaret Kenyatta.



Leo anatarajiwa kutembelea kituo cha wakfu wa kuhifadhi wanyama pori cha David Sheldrick kisha aelekee ikulu kwa mazungumzo. Baada ya hapo, atazuru Ukumbi wa Taifa wa Sanaa jijini Nairobi kujionea kazi za uigizaji na utamaduni wa Kenya.

Hapa chini anaonekana akipokea shada la maua kutoka kwa binti Mkenya, wanaotazama akiwa ni Mama Margaret Kenyatta na balozi wa Marekani Kenya Robert Godec.



Ndege aliyosafiria Bi Trump ilitua katika uwanja wa ndege wa Kimataifa muda mfupi kabla ya saa tatu usiku,  Kabla ya kusafiri kuja nchini Kenya, Bi Melania Trump alianza ziara yake katika bara hili huko nchini Ghana mapema wiki hii kabla ya kwenda Malawi.

Ziara ya Bi Melania Trump nchini Kenya inafuatia mashauriano waliyofanya na Mkewe Rais Margaret Kenyatta katika Ikulu ya White House wakati Mama wa Taifa aliandamana na Rais Uhuru Kenyatta katika ziara ya mwezi Agosti mwaka huu huko mjini Washington DC.



Hatua hiyo pia ilitokana na tangazo la Mkewe Rais wa Marekani wakati wa dhifa aliyoandaa kwa wajumbe waliohudhuria kikao cha 73 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambako alithibitisha ziara yake kwa mataifa ya Ghana, Malawi, Kenya na Misri.

Bi Trump atatamatisha ziara yake ya bara Afrika kwa kuzuru Misri.

Atazingatia zaidi huduma za afya kwa akina mama wajawazito na watoto wachanga, elimu na jukumu linalotekelezwa na Marekani Kenya kujitosheleza katika utoaji huduma.



Ajenda ya ziara ya Bi. Trump inawiana na harakati za shirika la Beyond Zero la Bi Kenyatta ambazo hushughulikia maslahi ya akina mama wajawazito, watoto wachanga, vijana waliobalehe, miongoni mwa masuala mengine mengi ya afya.



Leo Bi. Trump na mwenyeji wake Mkewe Rais Kenyatta watatafuta jinsi watakavyoimarisha ufungamano kati ya mashirika yao ambayo yanashughulikia masuala ya afya ya kina mama na watoto wachanga. Hii ni mara ya pili kwa wake hao wa viongozi kukutana, kwani mara ya kwanza walikutana Ikulu ya White House mjini Washington DC wakati wa ziara ya kiserikali ya Rais Kenyatta mwezi Agosti mwaka huu.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad