Mo Dewji: Maswali yanayogonga Vichwa Kutekwa kwa Tajiri Mkubwa Tanzania

 Kutekwa kwa tajiri Mo Dewji kumewaacha wengi katika lindi la mshangao na sintofahamu.

Kuna maswali kadhaa ambayo yamekuwa yakijitokeza toka iliiporipotiwa kutokea kwa tukio hilo Alhamisi alfajiri na kupatikana kwa majibu yake kunaweza kukatoa mwangaza wa kulielewa tukio lenyewe na pengine kupelekea kupatikana kwa tajiri huyo.

Kwanini ametekwa?

Baadhi ya vyombo vya habari vya kimataifa vimenukuu vyanzo kutoka jeshi la polisi Tanzania kuwa yawezekana kuwa Mo ametekwa kwa sababu za kifedha, ikihisiwa watekaji watadai komboleo ili wamuachie huru.

Mpaka sasa si familia wala mamlaka za nchi ambazo zimeeleza sababu rasmi ya tukio hilo. Hivyo haifahamiki ni kwanini tajiri huyo ametekwa.

Hatahivyo, kutokana na utajiri alonao (ambapo jarida la biashara la Forbes linakisia kuwa unafikia dola bilioni 1.5) ni jambo ambalo linayumkinika.

Nani amemteka?

Kauli rasmi ya mamlaka ambayo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam ni kuwa waliiongoza tukio hilo ni raia wawili wa kigeni.

Mashuhuda wanasema watu wanne wenye silaha walishiriki tukio hilo na walifunika nyuso zao. Mpaka sasa kuna watu 12 ambao wametiwa mbaroni kutokana na mkassa huo.

Uhusika wa wazungu hao wawili kwamujibu wa mamlaka unaashiria kuwa tukio hilo si dogo na ambalo lilipangiliwa vilivyo.

Kamanda Mambosasa ameibua maswali manne ambayo yanaonesha utata mkubwa wa namna tukio hilo lilivyotekelezwa.

Bosi huyo wa polisi wa jiji la Dar es Salaam ameliambia gazeti la Mwananchi kuwa maswali hayo yanawasumbua na wanatafuta majibu yake.

Swali la kwanza: "Hebu tujiulize kamera (iliyopo katika hoteli ya Colosseum) nayo imeshindwa kutupatia kila kitu kuna upande tumeshindwa kuupata vizuri tunajiuliza ilikwepeshwa makusudi?"

Swali la pili la Mambosasa linahoji kwanini walinzi wa hoteli ambayo Mo alitekwa hawakuwahoji wahalifu ambao walifika kabla ya Mo kutaka kujua kwanini hawakushuka kwenye gari walilokuwemo.

Swali la tatu: "Tunaambiwa wakati zoezi linafanyika hakukupigwa yowe wala majibizano ya risasi ina maana hawa waliokuwa hapa walilichukuliaje tukio hili?"

Katika swali lake la nne juu ya mazingira ya tukio Mambosasa amesema hakuna aliyeandika gari zinazoingia katika hoteli hiyo, "kwahiyo hebu tufanye uchunguzi."

Kwanini hakuwa na mlinzi?

Mo hakuwa na mlinzi wakati anatekwa, tena alikuwa akiendesha mwenyewe gari lake la kifahari wakati tukio hilo likitokea.

Hali hiyo imefanya watu wengi ndani na nje ya nchi kujiuliza kulikoni tajiri mkubwa wa aina yake amekosa kuambatana na mlinzi.

Wanaomfahamo Mo wanasema ni mtu asiye na makuu wala kujikweza. Mmoja wa wafanyakazi wake wa zamani ameiambia BBC kuwa si Mo wala wanafamilia wengine wa Dewji ambao wamekuwa wakitembea na walinzi.

Mara kadhaa dewji ameonekana akipanda usafiri wa kukodi wa pikipiki, maarufu kama bodaboda ili kuwahi aendako na kupambana na foleni kali ya jiji la Dar es Salaam.

Kwaujumla, ni nadra kukuta matajiri wakijihami na walinzi nchini Tanzania tofauti na ilivyo katika miji mingine mikubwa ya Afrika mathalan Lagos, Nigeria na Johannesburg, Afrika Kusini. Kwamujibu wa Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam hali hiyo inatokana na kuwepo kwa usalama ndani ya jiji na Tanzania kwa ujumla.

Lakini baada ya tukio la Mo, yamkini matajiri na vyombo vya dola vitaongeza kasi ya ulinzi ili kuepusha kujirudia kwa mkasa wa aina hiyo.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad