Rebeca Gyumi |
Rebeca Gyumi, mwanaharakati wa haki za wanawake na wasichana nchini Tanzania pamoja na watu wengine wawili na shirika moja la kiraia, wameshinda tuzo ya mwaka huu ya haki za binadamu
Washindi hao wametangazwa na Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Maria Fernanda Espinosa ambaye kupitia ukurasa wake wa Twitter amewapongeza kwa mchango wao wa kusongesha mbele haki za binadamu.
Hii ni tuzo ya 10 ambayo mwaka huu inaendana na miaka 70 ya tamko la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa ambapo washindi hao watapokea tuzo hizo tarehe 10 mwezi disemba mwaka huu kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani.
Taarifa ya ofisi ya Kamishna wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa imefafanua kazi za washindi hao akitolea mfano Rebeca Gyumi.
Bi. Gyumim muasisi na mkurugenzi mtendaji wa taasisi ya Msichana Initiative nchini Tanzania, kwa miaka 8 amekuwa akihoji uhalali wa ibara ya 13 na 17 ya sheria ya ndoa yam waka 1971 nchini Tanzania ambayo inahurusu mtoto wa kike kuolewa akiwa na umri wa miaka 14 na 15 kwa ridhaa ya wazazi au mahakama.
Taarifa hiyo inasema “Bi. Gyumi alishinda kesi hiyo mbele ya Mahakama Kuu ya Tanzaina mwaka 2016.” Mshindi mwingine ni Asma Jahangir mwanaharakati mwanasheria wa Pakistani ambaye amefariki dunia mwaka huu.
Marehemu Jahangir kwa miongo mitatu amekuwa akitetea haki za wanawake, wasichana, watoto na makundi madogo ya kidini na maskini nchini mwake ambapo alifungua kituo cha msaada wa sheria. Ingawa hivyo alikuwa akikumbwa na misukosuko lakini alikuwa na uwezo wa kushinda kesi zilizokuwa na utata.
Kwa upande wake, mshindi mwingine Joênia Wapichana au Joênia Batista de Carvalho, mwanaharakati wa haki za watu wa jamii ya asili nchini Brazil, ni mwanamke wa kwanza wa jamii hiyo kuwa mwanasheria. “Baada ya kuwasilisha mbele ya tume ya haki za binadamu ya nchi za Amerika, Bi. Wapichana alikuwa mwanasheria wa kwanza wa jamii ya asili kuingia Mahakama Kuu ya Brazil.