Musoma: Mke wa Mkuu wa Shule Ajifyungua Kokwa za Parachichi na Hirizi



Musoma, Mara.

Jumamosi 13, Oktoba 2018.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma Ndg. John Lipesi Kayombo amewataka Diwani wa Kata ya Bugoji, Mwenyekiti wa Kijiji cha Bugoji, Wenyeviti wa kamati za msingi Kanderema ‘A’ na ‘B’ pamoja na wananchi kuhakikisha ndani ya mwezi mmoja vitendo vya kishirikina vinavyoendelea katika shule hizo vinatokomezwa.

Mkurugenzi Kayombo ametoa maagizo hayo Jana Ijumaa 12, Oktoba 2018 wakati wa kikao cha pamoja kati yake na viongozi wa Kata ya Bugoji, viongozi wa Kijiji cha Bugoji, walimu wa shule za Msingi za Kanderema ‘A’ na Kanderema ‘B’ pamoja na wananchi wa Kijijij cha Bugoji.

Kikao hicho kimefanyika baada ya kuripotiwa matendo mengi ya kishirikina wanayokutana nayo walimu pamoja na wanafunzi wa shule hizo tangu mwaka 2013 mpaka sasa.

Matendo hayo ya kishirikina yaliyoripotiwa yakiwemo ya wanafunzi kuanguka darasani, kupotea kimazingara kwa vitu mbalimbali vikiwemo simu, mboga, kihifadhi chaji (power bank),kufunguliwa kwa milango, watoto wadogo kuwekwa uvunguni kimazingara, nyumba kufagiliwa na tukio kubwa la *mke wa Mwalimu Rawlence John ambaye ni Mkuu wa shule Kanderema ‘B’ kujifungua Kokwa za Parachichi zenye chale na hirizi nyeusi*.

Akizungumza wakati wa kikao hicho Mkurugenzi Kayombo aliwataka wananchi wa Kijiji cha Bugoji kuachana na dhana potofu ya ushirikina badala yake wawe msaada kwa walimu hao ili waweze kutimiza majukumu yao kiufasaha na hatimaye kuongeza ufaulu kwa wanafunzi.

“Nimesikitika kusikia mambo ya kishirikina yanayoendelea kufanyika hapa, madaftari yanasahihishwa kimazingara, watoto wanasweka uvunguni, milango inafunguliwa kimazingara, wanafunzi wanaanguka hovyo madarasani ikaenda mbali zaidi *mke wa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kenderema ‘B’ Mwl. Rawlence John kajifungua Kokwa mbili za Parachichi zenye chale na hirizi nyeusi* kwa Kweli sio jambo jema” alisema Kayombo.

“Uchawi wa namna hiyo katika karne hii haupo, tunahitaji uchawi wa maendeleo, tunahitaji hospitali, shule na barabara nzuri, huo ndio uchawi wa maendeleo” alisema Kayombo.

“Naagiza Mh. Diwani wa Kata ya Bugoji, Mwenyekiti wa Kijiji cha Bugoji, Wenyeviti wa kamati za shule za msingi Kanderema ‘A’ na Kanderema ‘B’ pamoja na wananchi muhakikishe swala hili ndani ya mwezi mmoja liwe limekwisha” alisema Kayombo.

Baada ya kumaliza kikao hicho Mkurugenzi Kayombo aliongoza na waalimu pamoja na viongozi wa Kijiji kwenda kuona nyumba wanazoishi walimu waliopatwa na maswahiba hayo.

Imetolewa na
Kitengo cha Habari na Uhusiano
Halmashauri ya Wilaya ya Musoma
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad