Paul Allen, bilionea aliyekuwa mmoja wa waasisi wa kampuni la Microsoft na Bill Gates mnamo 1975, amefariki dunia kwa kansa. Allen ambaye anakadiriwa kuwa na utajiri wa Dola bilioni 20 (Sh. tril. 45.7) alikutwa na umauti jana nyumbani kwake Seattle.
Wiki mbili kabla ya kifo, alikuwa ametangaza kuwa shambulio la kansa lilikuwa limemrudia baada ya kutulia kwa miaka tisa.
Allen na Gates, wote wakiwa hawakufanya vyema katika masomo yao chuo kikuu, walibuni wazo la kuanzisha kampuni ya Microsoft huko Albuquerque, Marekani. Walianzisha juhudi zilizozaa mapinduzi ya kompyuta.
Wawili hao walikutana na kuwa marafiki katika shule ya Lakeside School karibu na Seattle na kuanzisha urafiki na kuwa karibu zaidi kutokana na kupenda masuala ya kompyuta.
Allen aliyefeli masomo katika Chuo Kikuu cha Washington State, alimshawishi Gates washirikiane kutokana na yeye pia kutofanya vyema chuoni. Allen ndiye aliyebuni jina la Micro-Soft.
Kampuni hilo lilihamia huko Bellevue, Washington mwaka 1979. Aligundulika kuwa na kansa ijulikanayo kama ‘non-Hodgkin’s lymphoma’ mwaka 1983 ambapo alilazimika kujiuzulu nafasi yake lakini akibakia mjumbe kamili wa bodi ya kampuni hiyo hadi 2000.
Image result for Paul Allen
Allen alikuwa mpenzi wa muziki wa Jimi Hendrix, na alianzisha jumba la makumbusho la The Experience Music Project Museum huko Seattle.
Paul katika maisha yake ametoa zaidi ya Dola bilioni 2 (Sh. tril. 4.5) kwa ajili ya miradi mbalimbali ya kusaidia watu. Hakuwa na mke na hana watoto.