MWILI wa aliyekuwa mtangazaji wa vituo mbalimbali vya redio nchini na Ujerumani, Issac Gamba, utawasili kesho (Jumatatu) jijini Dar es Salaam saa nane za usiku kwa ndege ya Turkish Airline ukisindikizwa na mtangazaji Sudi Mnete.
Kwa mujibu wa waratibu wa shughuli hiyo, baada ya mwili huo kupokewa utapelekwa hospitali ya kijeshi Lugalo ambako ibada na shughuli nzima ya kumuaga itaanza saa tano asubuhi siku ya Jumatatu na baadaye utapelekwa uwanja wa ndege tayari kwa safari kuelekea Bunda kupitia Mwanza.
Ratiba Kwa Ufupi
Jumatatu Alfajiri – Kupokea mwili Airport
Jumatatu Kuanzia Saa Tano – Ibada na Heshima za Mwisho, Lugalo Hospital.
Jumatano – Mazishi Bunda.
A: KUZALIWA
Marehemu Isaac Nyagabona Muyenjwa Gamba, ni mtoto wa 12 kati ya watoto 13 wa familia ya marehemu mzee Elizaphan Munyenjwa Maribwa. Isaac alizaliwa Januari 19th 1970 wilayani bunda-mjini.
B: KUSOMA NA KAZI
Marehemu alipata elimu yake ya msingi, katika shule ya msingi Kabalimu iliyoko mjini Bunda kuanzia mwaka 1978 na kuhitimu mwaka 1984. Baada ya hapo, aliendelea na masomo ya sekondari katika Shule ya Sekondari Majengo Moshi kuanzia mwaka 1985 hadi mwaka 1988 na baadaye kuendelea na masomo ya A Level katika shule ya Old Moshi kuanzia mwaka 1989 hadi mwaka 1991.
Kisha akajiunga na mafunzo ya jeshi kwa mujibu wa sheria katika Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) mwaka 1991. Baadaye alipata mafunzo ya uandishi wa habari katika Radio Sauti ya Injili ya Mjini Moshi. Marehemu alifanikiwa kuhitimu elimu yake ya shahada ya Mass Communication katika Chuo cha Tumaini jijini Dar es Salaam mnamo mwaka 2010.
Marehemu alianza kufanya kazi kwa muda wa takribani miezi sita akiwa Arusha katika Radio 5, na ndipo kwenda kujiunga na kituo cha utangazaji cha Radio Free Africa (RFA) Mwanza mwaka 1997 mpaka mwaka 2003, kisha akajiunga na Radio Uhuru ya jijini Dar es Salaam mwaka 2004.
Mwaka 2005 alijiunga na kampuni ya IPP Media katika kituo chake cha habari cha Radio One na ITV hadi mwaka 2015 alipohamia katika shirika la utangazaji Ujerumani la Deutsche Welle (DW) ambapo mauti ilimfika akiwa huko.
C: MAISHA YA KIROHO
Gamba alikuwa ni mshiriki wa Kanisa la wa Adventista wa Sabato Mwenge jijini Dar es Salaam.
D: UGONJWA NA UMAUTI
Marehemu hakuwahi kuugua ugonjwa wowote wa kuaminika zaidi ya kukutwa akiwa amefariki chumbani kwake Oktoba 18 Alhamisi mwaka huu.
Baada ya uchunguzi wa hospitali nchini Ujerumani, imegundulika kuwa kilichosababisha kifo chake ni kuvuja kwa damu kwenye ubongo (Brain Hemorrhage) yaani presha ya damu.
Image result for Isaac Nyagabona Muyenjwa Gamba,
E: MAHUSIANO
Marehemu hakuwahi kuoa na hana mtoto au watoto wanaotambulika na familia.
F: SHUKRANI
Familia ya marehemu Mzee Elzaphan Muyenjwa Maribwa, inatoa shukrani kwa watu binafsi na taasisi kama ifuatavyo hapa chini.
i.Shirika la utangazaji la idhaa ya Kiswahili Ujerumani DW:
Familia inashukuru uongozi wote wa DW kwa kuguswa na kushtushwa sana na kifo cha marehemu na kwa jitihada zao walizofanya katika kufuatilia sababu za kifo cha marehemu pia kukubali kuusafirisha mwili wa marehemu kutoka Bonn, Ujerumani, hadi nyumbani kwao Bunda.
ii.Ubalozi wa Tanzania nchini Ujerumani:
Familia pia inashukuru Ubalozi wa Tanzania nchini Ujerumani kwa jitihada zao kwa kuhakikisha kwamba mwili wa marehemu unasafirishwa kurudi nyumbani kwao Tanzania.
iii.Uongozi wa IPP Media na wafanyakazi wake:
Familia inatoa shukrani kwa uongozi wa IPP Media na wafanyakazi wake kwa ushirikiano wao katika maandalizi ya kuuaga mwili wa marehemu.
iv.Wananchi wote wa Dar es Salaam, Bunda na Watanzania kwa ujumla:
Familia inatoa shukrani zao za dhati kwao kwa kuguswa kwa masikitiko makubwa na msiba wa ndugu yetu mpendwa Isaac.